WAZIRI WA AFYA AZINDUA MPANGO MKAKATI WA NNE WA VVU NA UKIMWI, AGPAHI YAISHUKURU SERIKALI


Serikali ya Tanzania imezindua Mpango Mkakati wa nne wa Virusi vya Ukimwi ‘VVU’ na Ukimwi katika sekta ya afya kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi hususani katika makundi ya watu walio katika hatari ya kupata maambukizi.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano Mei 9,2018 katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Chuo cha Mipango Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu.

Uzinduzi huo ulioambatana na sherehe za kutimiza miaka 30 ya Mpango wa taifa wa kudhibiti Ukimwi (NACP) umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya yakiwemo mashirika ya kitaifa na kimataifa yanayojihusisha ma mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini likiwemo shirika la AGPAHI.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango Waziri Ummy Mwalimu alisema mpango huo unaweka msisitizo katika kutoa huduma rafiki kwa vijana na makundi mengine katika jamii yaliyopo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU hasa wanaotumia dawa za kulevya, madereva wa magari ya masafa marefu, wavuvi na wafungwa.

“Mpango huu pia unaweka kipaumbele katika kuboresha huduma za kinga, tiba na matunzo sambamba na kuweka mazingira wezeshi ya kupata huduma hizo na kusisitiza na kuelekeza kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kutoa huduma za VVU na Ukimwi kwa watu waliopo katika wanaoishi na VVU”,alieleza.

Hata hivyo, aliyapongeza mashirika na taasisi mbalimbali zinazoendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwani Tanzania ya viwanda haiwezi kuwepo kama wananchi hawana afya bora.

“Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha Ukimwi unatokomezwa nchini na juhudi hizi zimekuwa zikilenga kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU”,alisema.

“Tumeweza kupunguza maambukizi ya VVU kitaifa kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 na sasa hivi tumefikia asilimia 4.7 kwa takwimu za mwaka 2016/2017”,alifafanua Waziri Ummy.

Alibainisha kuwa wakati maambukizi ya VVU yakipungua kitaifa katika mikoa 11 hali ya maambukizi yamepanda mfano; Tanga ilikuwa na maambukizi kwa asilimia 2.4% lakini sasa ni 5%, Dodoma ilikuwa na 2.9% sasa ni 5% na Mwanza 4.2% sasa imekuwa 7.2 %.

Aidha alisema maambukizi ya VVU yanaendelea kuwepo kutokana na wananchi wengi hususani wanaume kutojitokeza kupima afya zao hivyo ipo haja ya kuangalia namna ya kuwafikia watu hao.

“Changamoto kubwa ninayoiona sio watanzania wengi kupata maambukizi ya VVU bali ni watanzania wenye maambukizi ya VVU kutofahamu hali zao, kwani takwimu zinaonesha 48% ya Watanzania wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya VVU hawajui hali zao, tunachopaswa ni kuwafikia watu hawa ili tuwaingize katika programu za uanzishwaji na matumizi ya dawa za kupungua makali ya VVU (ART)",alisema.

Waziri Ummy alisema katika bajeti ijayo serikali imepanga shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kununua dawa za magonjwa nyemelezi ili kuboresha huduma za afya katika vituo vya tiba na matunzo nchini.

Waziri Ummy pia aliagiza kuanzia Julai 1, 2018 dawa zinazotolewa kwa watu wanaoishi na VVU zianze kutolewa kila baada ya miezi mitatu badala ya kila baada ya miezi ilivyo sasa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dkt. Sekela Mwakyusa aliishukuru serikali kwa kupanga bajeti ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kununua dawa za magonjwa nyemelezi kwani miongoni mwa changamoto kubwa katika vituo vya tiba na matunzo ni uhaba wa dawa hizo.

“Nimshukuru sana mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kutoa agizo la dawa za watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kupewa kila baada ya miezi mitatu, hii itapunguza mzigo wa wagonjwa kwenye vituo kwa sababu tumekuwa tukikabiliwa na changamoto hii kwenye vituo vya tiba na matunzo”,alisema.

Alisema kitendo cha kutoa dawa kila baada ya miezi mitatu mbali na kusaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa, pia watoa huduma watafanya kazi zingine na kuepusha usumbufu kwa wateja waliopo katika huduma.

Aliongeza kuwa ili kuwafikia Watanzania waliopo katika 48% ambao hawafahamu hali zao kiafya,shirika la AGPAHI linaendelea na mikakati ya kuyafikia makundi maalumu.

“Sisi kama wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, tunaendelea na jitihada za kuwapata wateja kwa kuyafikia makundi yanayotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuwapima watoto wa wateja na kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa rafiki kwa wanaume ikiwemo kuongeza muda wa kliniki”,alieleza Dkt. Sekela.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo kwenye chuo cha Mipango jijini Dodoma - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimuakizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Meza kuu wakiwa ukumbini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dkt. Sekela Mwakyusa akipunga mkono ukumbini baada ya kutambulishwa kuwa shirika lake ni miongoni mwa wadau wakubwa katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini Tanzania.
Wadau wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Zainabu Chaula akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Afisa Mawasiliano shirika la AGPAHI,Glory Macha akiandika dondoo muhimu wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu akizindua Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akiangalia kitabu cha mwongozo wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na viongozi mbalimbali wakiwa wameshikilia vitabu vya mwongozo wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi.
Wadau wa afya nchini hususani wanaojihusisha na mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi wakiwa wamesimama ukumbini wakati wa zoezi la uzinduzi wa wa Mpango Mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akikata keki wakati wa sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiteta jambo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa.
Wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi wakipiga picha ya kumbukumbu na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Wadau wakiendelea kupiga picha na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi wakipiga picha ya kumbukumbu na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Zainabu Chaula.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527