SIMBA KUBEBA KOMBE SIKU YA MAFISANGO


Kiungo wa zamani wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango ke­sho Alhamisi anatimiza miaka sita kaburini katika wiki ambayo Simba inabeba kombe jingine tangu yeye afariki.

Simba haikuwahi kubeba Kombe la Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2012 ambao Mafisango alikuwa kikosini na kupachika mabao 12 akicheza kama kiraka.

Simba ambayo msimu huu imetwaa ubingwa bila kupoteza mchezo itakabidhiwa kombe lake Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar ya kipa Juma Kaseja ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafisango.

Jumapili hiyo itakuwa Mei 20, am­bayo ndiyo siku ambayo Mafisango aliyefariki Mei 17 mwaka 2012, alizikwa majira ya saa 11 jioni kwenye makaburi ya Lemba, nje kidogo ya Jiji la Kinshasa. Hivyo Simba wakati wakijiandaa kubeba Kombe lao mida hiyo ya jioni Mafisango atakuwa akitimiza miaka sita ndani ya kaburi pale Kinshasa.

Mafisango ambaye alikuwa na uraia wa DR Congo na Rwanda, alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Keko jijini Dar es Salaam wakati akitokea kwenye starehe kurejea nyumbani kwake tayari kwa safari ya kurudi kwao Rwanda kujiunga na kambi ya timu ya Taifa.

Moja ya vitu ambavyo vilishangaza Watan­zania wengi kwenye maziko ya mchezaji huyo ni staili ya washikaji zake kupitisha jeneza lake kwenye vijiwe vyake vyote kuaga ndugu na rafiki zake ikiwemo Baa kabla ya kuun­ganisha makaburini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527