SERIKALI YAWAPA SIKU TATU WAFANYABIASHARA KURUDISHA SUKARI NA MAFUTA MTAANI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na kwa bei ya kawaida.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni Mei 9, 2018 Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.

"Natoa siku tatu kuanzia kesho Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi mafuta yote yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee kusambazwa kama kawaida nchini kote ili kuondoa uhaba uliojitokeza na kamwe Serikali haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu", amesema Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema "kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo".

Waziri Mkuu amesema takwimu zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini yanatosha, hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba. 

"Hatuwezi kukubaliana na jambo hili kwa sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango uliopangwa kwani imekuwa ni kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo Serikali haitakubali wananchi wateseke bila sababu za msingi," amesisitiza. 

Akiwasilisha kauli ya serikali Bungeni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Mwijage amesema vyanzo vinavyotumika kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa asilimia 30, hivyo asilimia 70 ya mafuta huagizwa kutoka nje ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527