MTOTO WA BABA WA TAIFA 'NYERERE' AMSHANGAA RAIS MAGUFULI


MTOTO wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, amesema ameshangazwa na uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli kumteua kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM) kwa kuwa hakuwahi kuwaza kupata nafasi hiyo. 

Makongoro ambaye ni mtoto wa nne kuzaliwa kwa Baba wa Taifa anakuwa wa kwanza katika familia hiyo kuwa mjumbe wa NEC.

Mwenyeti wa CCM, Rais Magufuli, jana alitangaza kuwateua Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere kuwa wajumbe NEC.

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Makongoro alisema: “Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wangu wa chama amenishangaza kati ya nafasi zake zisizozidi saba za kuteua wajumbe wa NEC ameniteua na mimi.”

“Amenipa heshima kubwa sana kuniteua katika nafasi zake za kwanza tena na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ambaye ni kiongozi ninayemheshimu sana,” alisema Makongoro.

Alisema Rais Magufuli mara kwa mara amekuwa akitoa ahadi kwa Watanzania kuwa hatawaangusha katika utendaji kazi wake na hivyo kumteua kwake ni heshima kubwa.

“Si tu kunipa heshima bali pia ameona ninafaa na mimi naahidi sitamuangusha kwa sababu ameona namimi naweza kutoa mchango wangu katika vikao vya juu vya chama,” alisema.

Kuhusu uteuzi huo, Makongoro alisema hakuwa anafahamu jambo lolote na wala hakutarajia kupatiwa nafasi hiyo ya juu.

Alisema amekuwa akijishughulisha na kazi zake binafsi katika kipindi cha mwaka mmoja tangu akose nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki, mwaka jana.

“Nimekaa benchi kwa muda mrefu sasa na nimekuwa nikiendelea na shughuli zangu binafsi mkoani Morogoro huku nikiendelea kujifua na mazoezi kwa ajili ya kuwa mchezaji wa akiba” alisema huku akicheka.

Makongoro pia alisema neema ya uteuzi huo imekuja wakati ambao ni msimu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaowalazimu Waislam kote nchini kufunga ili kutimiza nguzo za dini hiyo.

“Kweli nimeamini mwezi Mtukufu wa Ramadhani upo, Nimeshuhudia Ramadhani nyingi wakati nasoma na hatua nyingine katika maisha yangu, lakini hii ya mwaka huu ni historia sitausahau mwezi huu mtukufu wa Ramadhani,” alisema Makongoro.

Kadhalika, Makongoro aliahidi kuwa mtumishi na mwanachama mwaminifu wa CCM na uadilifu mkubwa.

“Katika utumishi wangu kwa nafasi niliyoteuliwa ya mjumbe wa NEC nitakuwa mwadilifu kwa kuwasilisha matatizo ya wanachama na kuhakikisha yanasikilizwa na kufanyiwa kazi,” alisema Makongoro.

Aprili 24, mwaka huu, wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa benki ya NMB mkoani Dodoma, Makongoro alimwomba Rais Magufuli ampe kazi kwa sababu yeye ni mchezaji wa akiba akisubiri kuanza kazi.

Aliposimama kuzungumza kwenye tukio hilo, Rais Magufuli alisema Makongoro anastahili kuwa mchezaji wa nafasi ya kwanza na si mchezaji wa akiba.

Makongoro Nyerere ni nani?

Alizaliwa Januari 30, mwaka 1959 na katika maisha yake siasa aliwahi kujiunga na chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995.

Mwaka huo huo alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kwa tiketi ya chama hicho, lakini alidumu kwa miaka miwili katika nafasi hiyo.

Mwaka 1997 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitengua ubunge wake na uchaguzi uliofuata Felix Mrema wa CCM alichukua nafasi hiyo.

Mwaka 2000 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya baba yake Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere kufariki, alijiunga na CCM.

Mwaka 2004 Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alimteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 2007 akiwa kada wa CCM, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara nafasi aliyodumu nayo hadi mwaka 2012.

Mwaka 2012 Makongoro, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kati ya wabunge nane kutoka Tanzania.

Mwaka 2015 Makongoro alikuwa miongoni mwa vigogo 38 wa CCM waliochukua fomu ya kutaka kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi ya urais ingawa hakufika mbali.

Chanzo- Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527