MFANYAKAZI WA MAMLAKA YA MAJI KAHAMA AFARIKI KWA KUTUMBUKIA MTARONI


Rexpirius Vicent Ntukigwa enzi za uhai wake


Mfanyakazi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Kahama (KUWASA) Rexpirius Vicent Ntukigwa (29) ambaye ni mkazi wa Nyahanga mjini Kahama mkoani Shinyanga amefariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa anaendesha kuacha njia na kutumbukia mtaroni.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule tukio hilo limetokea jana Mei 23,2018 majira ya saa 12 na dakika 45 asubuhi katika eneo la Five Ways - Nyihogo barabara itokayo Kahama Mjini kuelekea Zongomela kata ya Igalilimi mjini Kahama.

"Pikipiki yenye namba za usajili SU 40403 aina ya Boxer mali ya KUWASA ikiendeshwa na Rexpirius Vicent Ntukigwa ambaye ni mtumishi wa KUWASA,iliacha njia na kutumbukia mtaroni na kumsababishia majeraha makubwa kichwani na kiunoni na kukimbizwa hospitali ya Mji wa Kahama kwa ajili ya matibabu",ameeleza Kamanda Haule.


"Tarehe 24,2018 majira ya 6 usiku majeruhi huyo alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu",ameongeza.

Aidha amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mwendesha pikipiki huyo aliyekuwa amelewa.

Msemaji wa KUWASA, John Mkama amesema mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea kwao mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527