DC NDAGALA AWAPA KIBANO WALEVI AKIKAGUA SHUGHULI ZA MAENDELEO KATA YA MUHANGE KIGOMA

Ulevi kupita kiasi ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha  maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla hali inayosababisha mambo mengi ya maendeleo kushindwa kukamilika kwa wakati kutokana na baadhi ya wananchi kuanza kunywa pombe za kienyeji kuanzia asubuhi na kushindwa kufanya shughuli yoyote jambo ambalo linapigwa vita na viongozi wa serikali.

Hali hiyo imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala ,kuwaagiza askari polisi kuwakamata watu wote waliokuwa wanakunywa pombe katika vilabu vya pombe ya kienyeji ikiwa ni pamoja na kuwanyang'anya vitambulisho vyao askari wawili wa jeshi la Akiba (Mgambo)  katika Kijiji cha Muhange kata ya Muhange waliokuwa wakinywa pombe kuanzia asubuhi, alipofika kijijini hapo jana kwa ajili ya kukagua na kuunga mkono shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo.

Alisema anasikitishwa kuona watu wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo na kuanza kunywa pombe asubuhi na wengi wao wakiwa ni vijana wakati wenzao wakijitolea katika ujenzi wa shule ya Sekondari ili kuweza kutatua changamoto ya wanafunzi wa kata hiyo kutembea umbali mrefu ili kufuata shule ilipo ambapo wananchi wameanza juhudi zao na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wananchi.

Aidha Mkuu huyo aliwataka wenyeviti wa vijiji vyote kuhakikisha vilabu vya pombe vyote vinafunguliwa kuanzia saa kumi jioni baada ya watu kumaliza kazi zao na wazingatie hilo na kuendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote wanaokiuka sheria hiyo kwani ndiyo chanzo cha kuwa vibaka na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na serikali kwa ujumla.

" Ni aibu sana kuona vijana wadogo ambao mnanguvu za kufanya kazi kuja kunywa pombe asubuhi mnashindwa kufanya kazi, afisa wa polisi hakikisha unawakamata hawa wote wanaokunywa na waliolewa muda wa kazi, sisi tunakuja kuhimiza maendeleo, wao wanaendelea kuturudisha nyuma.

 Niwaombe wazazi mkae na watoto wenu muwafundishe na kuwaonya hatuko tayari kuona Wwlaya yetu inaendelea kuwa maskini lazima tuhakikishe watu wanafanya kazi na muda wa kunywa pombe ni jioni, nikiwakuta tena nitawachukulia hatua kali za kisheria", alisema Kanali Ndagala.

Sambamba na hayo Kanali Ndagala alishiriki katika ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Muhange pamoja na shughuli mbali mbali za maendeleo,na aliahidi kuongeza mifuko kumi ya saruji na kuwahakikishia kuwa serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na kuwaasa wananchi kuiga mfano huo kwa kuunga mkono jitihada za serikali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Muhange Ibrahim Katunzi alimpongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa namna anavyojitahidi kuhimiza maendeleo katika wilaya hiyo ambayo ilikuwa nyuma kwa kila kitu lakini kwa sasa inaendelea kuwa vizuri na miradi mingi inakamilika ikiwa ni pamoja na wananchi kujitolea kwa uaminifu kwa kuamini serikali ni sikivu.

Alisema yeye kama mwakilishi wa wananchi atahakikisha anahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kufanya kazi ili kuhakikisha huduma muhimu zilizokosekana katika kata hiyo wanafanya kwa ushirikiano kuhakikisha zinapatikana.

Mmoja wa wananchi hao,Wiston Joramu alisema changamoto waliokuwa nayo ni watoto kutembea umbali mrefu kwa miguu na ukizingatia maeneo mengi kuna mapori hali inayosababisha usalama wa watoto wao kuwa hatarini na wamelazimika kujenga shule hiyo ili kutatua changamoto hiyo.

Na Rhoda Ezekiel -Malunde1 blog
ANGALIA PICHA

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Muhange kata ya Muhange waliokuwa wakinywa pombe kuanzia asubuhi, alipofika kijijini hapo jana kwa ajili ya kukagua na kuunga mkono shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Muhange
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Muhange
Wananchi waliokutwa wakinywa pombe
Kibano baada ya kukutwa wakinywa pombe
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akiwa ameshikilia pombe
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akishiriki ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Muhange



Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akishiriki ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Muhange.Picha zote na Rhoda Ezekiel -Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527