WANANCHI KIBONDO WAELEZA KUTORIDHISHWA NA UPATIKANAJI WA DAWA JAPO WANA KADI ZA BIMA YA AFYA


Wakazi wa kijiji cha Mabamba kata ya Mabamba wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma wameeleza kutoridhishwa na huduma ya upatikanaji wa dawa katika kituo chao cha afya cha Mabamba wilayani Kibondo licha ya kuwa na kadi za bima afya na hivyo kuiomba serikali kuwatatulia tatizo hilo.

Wakizungumza wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru baadhi ya wakazi hao akiwemo Ester Honoli na Gloria Razalo wamesema mara kadhaa wanapofika katika kituo hicho cha afya kupata huduma za matibabu huwa hawapatiwi dawa na kuambiwa wakanunue katika maduka ya madawa.

"Tukipata matibabu daktari akituandikia dawa mara nyingi tunaambiwa hazipo na dawa ambazo zinapatikana ni zile za bei ya chini kama mseto na asprini na wakati tuna bima na hivyo tunalazimika kununua dawa kwenye maduka ya madawa",walisema.

Aidha mganga mfawidhi wa kituo hicho Primus Ijuma alisema dawa zipo kwa wingi tangu Januari mwaka 2018 na wagonjwa wanapatiwa isipokuwa kuna baadhi ya dawa huwa zinakosekana katika kituo hicho.

Akizungumzia hilo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa kwa mwaka 2018 Charles Kabeho aliwaagiza maafisa TUKUKURU wilaya kuchunguza ununuzi na uuzwaji wa dawa katika kituo cha  Mabamba kwa kuwa wananchi wanalalamika wakati Mganga wa hospitali hiyo anadai kuwa tangu mwezi wa Kwanza wamekuwa wakipokea dawa za kutosha.

Kiongozi huyo alisema serikali inatoa dawa za kutosha hivyo ni wajibu wa mamlaka husika kuhakikisha dawa zinatolewa kwa wagonjwa na kwa wakati huku akiitaka mamlaka ya kudhibiti rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi kuhusu dawa zinayofikishwa kituoni hapo yanatumikaje.

"Wananchi wanaeleza wazi hawapati dawa mara wanapofika kituoni jambo ambalo linasababisha kero na usumbufu kwa wananchi . Naomba TAKUKURU mfuatilie kujua dawa zinatumikaje lakini pia huko wanapoambiwa wakanunue dawa ni duka gani wananunua, na je linauhusiano wa yeyote katika kituo cha afya, kisha nipate taarifa ndani ya siku kumi na nne" alisema Kiongozi huyo.

Naibu waziri uchukuzi na mawasiliano wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye alisema serikali ina lengo kubwa la kuboresha huduma za kijamii ambapo kituo hicho kilipatiwa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, vifaa tiba pamoja na vitenganishi vinavyotumika maabara.

Naibu waziri huyo alisema mbali na uboreshaji wa huduma za afya lakini pia serikali itahakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana pamoja na nishati ya umeme kupitia huduma ya umeme vijijini Rea 

Mwenge wa uhuru umewasili wilaya ya Kibondo mkoa wa Kigoma ukiwa ukitoe wilaya ya Kakonko ambapo Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amemkabidhi mkuu wa wilaya ya Kibondo Louis Bura ambaye alieleza jumla ya miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja itazinduliwa,kukaguliwa na kuwekewa jiwe la msingi 

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akimkabidhi Mwenge wa uhuru mkuu wa wilaya ya Kibondo Louis Bura . Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527