WANACHAMA NA VIONGOZI WA CHADEMA WAFURIKA MAHAKAMANI KUSUBIRI HATMA YA MBOWE NA WENZAKE


Wanachama na viongozi wa Chadema wamekusanyika ndani na nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusubiri hatma ya dhamana ya viongozi wakuu wa chama hicho.


Viongozi hao, Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe na wenzake watano wanatarajiwa kuachiwa kwa dhamana leo iwapo watatimiza masharti ya dhamana.


Masharti hayo ni kusaini bondi ya Sh20milioni kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka ofisi za Serikali za mitaa au vijiji na kuripoti kituo kikuu cha Polisi kila Alhamisi.


Tayari Mbowe na wenzake wameshafikishwa mahakama ni tangu saa mbili asubuhi hii na sasa wanasubiri shughuli za kimahakama zianze ili wakamilishe masharti ya dhamana.


Mbali ya Mbowe wengine ni Katibu Mkuu Dk Vicent Mashinji, Manaibu Katibu wakuu John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake wa chama hicho Ester Matiku wanakabiliwa na kesi ya jinai, wakidaiwa pamoja na mambo mengine ikiwamo kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali.


Wamekuwa mahabusu tangu walipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo Machi 27 mwaka huu, 2018.


Na James Magai, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527