SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI AZUIA WABUNGE WASIPAPASWE


SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameagiza mamlaka za usalama ziache kukagua wabunge kwa kuwapapasa wanapoingia bungeni.

Ndugai amesema bungeni kuwa, haiwezekani wabunge waendelee kupapaswa na kwamba, hiyo ni njia ya kizamani ya kufanya kazi.

"Waache kupapasa wabunge wangu, haiwezekani, haiwezekani..." amesema Ndugai wakati anatoa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Kavuu (CCM), Pudenciana Kikwembe.

Ndugai pia amesema, hakuna haja ya wabunge kuwa na vitambulisho kwa kuwa wanapoingia bungeni picha zao zinaonekana.

Amesema, kwa namna jambo hilo lilivyozungumzwa inaonekana linawakera wabunge likiwemo suala la vitambulisho na ukaguzi milangoni. Ndugia amesema, Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai amesikia hivyo malalamiko yafanyiwe kazi.

Wakati anaomba mwongozo, Kikwembe amesema, mchakato wa sasa wa kukagua wabunge ni sawa na kuwavua nguo.

Amesema, mwili mwa mwanadamu una vivutio vingi, na kwamba yeye amekaguliwa kwa kushikwashikwa kwa mikono.

Amepinga kukaguliwa kwa namna hiyo hasa ikizingatiwa kuwa, wapo Dodoma kwa muda mrefu, wameacha familia zao mbali hivyo wakishikwashika inaweza kuwapotezea mwelekeo wanapoingia bungeni.

Amesema ukaguzi wa sasa ni kutiana hamasa bila sababu za msingi.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara ameomba mwongozo wa Spika kwa kusema, kuwapa wabunge vitambulisho kama watoto imepitwa na wakati, na kwamba, badala ya kwenda mbele kwenye mambo ya usalama Bunge linarudi nyuma.

IMEANDIKWA NA BASIL MSONGO - HABARILEO DODOMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527