SERIKALI YAMJIBU RASMI ZITTO KABWE ,YAELEZA KWA KIREFU TRILIONI 1.5 ZILIVYOTUMIKA


 Serikali imetoa mchanganuo wa Sh 1.5trilioni zinazodaiwa kutojulikana zilipo.

Akizungumza bungeni leo Aprili 20, Naibu Waziri wa Fedha amesema kiasi cha Sh697 bilioni kilitumika katika matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva, Sh 687bilioni kwa ajili ya mapato tarajiwa na Sh 203 bilioni ni za mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar.

Kutolewa kwa majibu hayo na Naibu Waziri, kulikuja baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kukatisha kipindi cha maswali na majibu na kuipa  serikali nafasi ya kutoa hoja ya kutoonekana kwa Sh 1.5 trilioni kwenye matumizi ya Serikali.

Naibu Spika amesema bungeni hapo, maswali na majibu yatapangiwa utaratibu mwingine.

“Hakuna Fedha kiasi cha Sh1.5trilioni iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge tukufu. Madai ya watu wasiyoitakia mema nchi kuhusu matumizi ya fedha hii hawana nia njema na nchi,”amesema Dk Kijaji

Amesema kutoonekana kwa fedha hiyo kulitokana na taarifa ya ukaguzi ya CAG kutumia taarifa za hesabu za nyaraka mbalimbali na hivyo kutojumuishwa kwa baadhi ya taarifa za utekelezaji wa bajeti.

Amesema hadi kufikia Juni 2017, mapato yalikuwa Sh 25.3 trilioni na matumizi yalikuwa Sh23.79 trilioni.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh 697.85bilioni zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za serikali zilizoiva,” amesema

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe,  alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa katika ukurasa wa 34 wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali, (CAG)Sh 1.5 trilioni hazikutolewa kwa matumizi wala kukaguliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527