NAPE NNAUYE AILIPUA SERIKALI BUNGENI

Mbunge Nape Nnauye amefunguka na kuibana serikali ya awamu ya tano kupitia Waziri wake Mkuu kuwa kitendo cha hotuba yake Bungeni kutokuwa na hata neno moja linalohusu gesi ni usaliti mkubwa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara kwa kudai gesi ndiyo yalikuwa makubaliano yao wakati wa kupiga kura.

Nape ametoa kauli hiyo leo Aprili 09, 2018 Bungeni katika mkutano wa 11 kikao cha tano cha Bunge la 11 linaloendelea kufanyika Mjini Dodoma baada ya kuipitia hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inatakiwa kusomwa mbele ya Wabunge huku ikiwa haina hata neno moja kuanzia mwanzo wa ukurasa hadi mwisho linaloshabiana na gesi na mafuta.

"Tulipopiga kura mwaka 2015, tuliamini kwamba uchumi wa gesi kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni ukombozi mkubwa na upo salama mikononi mwa Rais Magufuli na serikali ya awamu ya tano. Tulipopiga kura ndio ukawa mkataba wetu siyo kwa maneno, kwa hiyo kura alizozipata Rais Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano yaliyopo ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo ndani yake kuna masuala ya gesi kwamba atakwenda kuyaendeleza", amesema Nape.

Pamoja na hayo, Nape ameendelea kwa kusema "hivi ni bahati mbaya kwamba hotuba ya Waziri Mkuu imeshindwa kuliona jambo hili kuwa ni kubwa na ikaamua kuliacha au serikali imeamua kuachana nalo kwa sababu naona jitihada kubwa zinaenda kwenye umeme wa maji lakini umeme wa maji katika ilani haumo. Ilani tumezungumza nishati ya gesi tena kwa sehemu kubwa sana. Hii ndio ilikuwa imani ya wanalindi na mtwara kwa serikali ya awamu ya tano".

Aidha, Nape amesema wakati mchakato wa kupata madini hayo katika mkoa wa Lindi na Mtwara wananchi wengi walipoteza maisha yao huku wengine wakipata ulemavu na majeraha mbalimbali ili mradi kuiwezesha nchi yao iwe na nishati ya gesi na mafuta.

"Kuna mali za watu zilipotea lakini tukaamini kuna neema kesho yake. Jambo hili bahati mbaya tulimkabidhi sisi Rais Magufuli tukaamini lipo salama, alipotupa Majaliwa tukaamini tupo salama zaidi kwa sababu Waziri Mkuu ametoka kwetu. Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa neno gesi maana yake ni kwamba hili jambo limeanza kuachwa sasa ili tuende kwenye umeme wa maji. Lakini je hatusaliti Ilani ya uchaguzi CCM pamoja na wananchi wa Lindi na Mtwara waliotupa kura na kutuamini kwamba gesi na uchumi wao upo salama?", amehoji Nape.

Nape ameendelea kusisitizia
"Hili ni bomu kubwa, wakati wa mchakato hali ya kisiasa, kijamii Lindi kulikuwepo na tabu sasa imetulia tukiamini neema ipo lakini kiuchumi baada ya harakati za gesi na mafuta kusini watu walianza kuekeza na uchumi ulikuwa, ila hali ya sasa waekezaji wanaondoka na uchumi umeanza kudorola, hali yetu ngumu sana".

Kwa upande mwingine, Nape amemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asikubali suala la gesi lisiwe mikono mwake yeye akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527