HATMA YA KESI YA MBOWE NA WENZAKE KUJULIKANA MEI 15

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia May 15,2018 kutoa uamuzi wa kesi ya kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali inayowakabili viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe kama iende Mahakama Kuu ama laa.


Hatua hiyo inatokana na mvutano wa hoja za kisheria zilizotolewa jana na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kisha kujibiwa leo na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.


Katika majibu yake Wakili Nchimbi ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali hoja za utetezi zilizotolewa na Kibatala kwa sababu zitapelekea ucheleweshaji wa shauri hilo pasipokuwa na sababu za msingi.


Nchimbi amedai kuwa katika mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo toka ilipoanza hadi leo hakuna swali lolote la msingi lililoibuliwa na upande wa utetezi ambalo linajikita na uvunjifu ama ukiukwaji wa haki ya kikatiba.


“Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia msingi wa hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi jana zimejikita katika mashtaka yanayowakabili washtakiwa” -Nchimbi


Alibainisha kuwa ukiangalia mlolongo wa hati ya mashtaka ni hati ambayo washtakiwa wamesomewa mashtaka zaidi ya mara moja ama mbili ikiwamo jana na washtakiwa waliyasikia mashtaka, wakayaelewa ndiyo maana wakaenda mbele wakayakanusha.


“Kama kweli washtakiwa waliona mashtaka haya siyo halali, hati ya mashtaka ilitolewa mapema hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zingewasilishwa kabla washtakiwa hao hawaja enterpre,” -Nchimbi.


Nchimbi amedai kuwa washtakiwa wamefunguliwa kesi ya jinai wakati walikuwa katika mkutano halali wa kampeni ya uchaguzi mdogo na kwamba kuwafungulia mashtaka hayo ni uvunjifu wa haki ya kikatiba, alisisitiza kuwa ni rai ya upande wa mashtaka kwamba yote yaliyoongelewa na upande wa utetezi hayawezi kuitwa ni maswali ya kikatiba ambayo yangeilazimu mahakama kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.


“Hakuna suala la kikatiba hapa na ukiendelea kufuatilia hoja za utetezi hawajashambulia vifungu vya kisheria vilivyotumika kuwashtaki washtakiwa hao, hivyo hoja zao hazina mashiko.” -Nchimbi


Baada ya kutolewa kwa hoja hizo,Wakili Kibatala aliiaambia mahakama kuwa mchakato wa kijinai ni mchakato mtakatifu ambao haukukusudiwa kuwashtaki watu ambao wanatekeleza majukumu yao kikatiba.


Kibatala alisisitiza kuiambia mahakama kuwa wanataka kwenda Mahakama Kuu ili kupata tafsiri ya je ni kweli mtu akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikatiba ashtakiwe kijinai.


Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi May 15,2018 kwa ajili ya kutoa uamuzi kama kesi hiyo iende Mahakama Kuu ama lah.


Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.


Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, Katibu wa chama hicho Dk Vicenti Mashinji, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa Tarime vijijini, John Heche na mbunge wa bunda, Ester Bulaya.


Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527