WANAUME WANAOKOPA BILA KUWASHIRISHA WAKE ZAO KUKIONA CHA MOTO


Serikali imewapiga marufuku wanaume wanaotumia mali za familia kama dhamana za mikopo bila kuwashirikisha wake zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria, kanuni na taratibu za ndoa nchini.


Hayo yamesemwa leo Machi 8 na mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Daqarro kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.


Daqarro amesema kuwa wapo wanaume wanaotumia mali za familia kama nyumba kukopa bila kuwashirikisha wake zao na wakishindwa kulipa mikopo, mali ya familia hupigwa mnada.


“Niwakaribishe kwangu mje mtoe taarifa endapo ukigundua mume wako amechukua mkopo na kuweka dhamana mali ya familia kati ya nyumba, gari, shamba au chochote nawaahidi nitasema nao kwa mujibu wa sheria maana ndio wanaotujengea wingi wa watu tegemezi baadae,” amesema.


Mbali na hilo amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia na mila potofu hasa za umiliki wa ardhi na mali za familia lakini pia kuungana kwa pamoja.


“Nguvu ya kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia iko mikononi mwenu wanawake kwa kupendana na kuacha husuda na chuki za waziwazi baina yenu, badala yake muwezeshane maana mafanikio ni kumiliki uchumi lakini pia kupendana kwani wengine wanaotekeleza ukatili huu kwa mwanamke ni wanamke wenyewe,” amesema Daqarro na kuongeza:


“Ukomavu wa kumiliki uchumi ndio nguvu ya mwanamke na silaha pekee ya kupinga ukatili hivyo wajengeeni watoto wenu wa kike hili tangu wadogo huku mkiwapa elimu maana ndio nguzo kuu ya familia na jamii, mkitimiza haya yote basi ukatili na unyanyasaji mtakuwa mmeutokomeza maana hamtakuwa mnategemea kuwezeshwa bali kuwezesha.”


Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia amesema kuwa zaidi ya vikundi 110 vya wanawake vimewezeshwa mikopo ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa lengo la kuwapa fursa ya kutekeleza nchi ya viwanda katika vikundi vya ujasiriamali.


Na Bertha Ismail, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527