WANAFUNZI WATOA MSAADA KWA WAZEE KUNYEMELEA BARAKA WAFAULU KWENYE MTIHANI WA TAIFA

Watahiniwa wa kidato cha sita katika shule ya “New Age open”ya jijini Tanga,jana Machi 16, walitoa msaada wa vyakula,sabuni,nyavu za mbu na simu kwa wazee walioathirika na ukoma wa kituo cha Misufini Wilayani hapa ili kupata baraka zao kabla ya kufanya mtihani wa kitaifa Mei mwaka huu.

Watahiniwa hao 29 wamefanya hivyo wakifuata nyayo za watangukizi wao 35 waliofanya mitihani kama hiyo mwaka jana waliopeleka msaada kama huo na kujikuta wakipata ufaulu wa kuwawezesha wote kupata mkopo wa Serikali katika vyuo vikuu walivyochaguliwa.

Wakizungumza wakati wakikabidhi msaada huo watahiniwa hao wamesema licha ya kwamba walimu wao wamefanya kazi ya ziada kuwafundisha itakayohakikisha wanafanya vyema mitihani ya kujiunga na elimu ya juu lakini baraka za wazee hao waathirika wa ukoma zina umuhimu wa aina yake.

“Tumekuja hapa tukiamini kwamba wakifurahi wazee hawa kwa ajili yetu watatupa baraka za kutuwezesha kufanya vyema mitihani ya Taifa ya kidato cha sita na kwenda vyuo vikuu wote”amesema Shedrack Mnzava ambaye ni kiongozi wa wanafunzi hao wa kidato cha sita.

Msaada waliotoa wanafunzi hao ni mikate,nyembe,wavu wa mbu wa kuweka madirishani,sembe sukari,sabuni pamoja na simu vyote vikiwa na thamani ya sh 500,000.

Na Burhani Yakub,Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527