TUNDU LISSU ASEMA SAKATA LA MBOWE NA VIONGOZI WA CHADEMA NI MAANDALIZI YA UPINZANI KUELEKEA IKULU

Siku moja baada ya viongozi sita wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kushtakiwa kwa makosa manane na kukosa dhamana, Tundu Lissu amesema kitendo hicho ni maandalizi ya upinzani kuelekea Ikulu.

Akizungumza leo Jumatano Machi 28, 2018 na MCL Digital, mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) aliyeko nchini Ubelgiji kw amatibabu, Lissu amesema kilichowapata viongozi hao hakiwezi kuzima madai ya kudai demokrasia.

Viongozi hao wamelala mahabusu wakikabiliwa na mashtaka manane ikiwamo kufanya uasi, kuhamasisha chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi, Akwilina Akwilini.

Pamoja na Mbowe, viongozi wengine ni katibu mkuu, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu (Bara), John Mnyika, naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.

“Ukandamizaji huu ni maandalizi tu ya kwenda Ikulu. Hawatafanikiwa kuzima moto wa madai ya demokrasia na haki za binadamu,” amesema Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema.

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527