TUNDU LISSU :KUSHIKILIA VIONGOZI WA CHADEMA NI KUWAPA UPAKO MKUBWA WA KISIASA MBELE YA WANANCHI

Mbunge wa Singida, Tundu Lissu amesema kitendo cha viongozi wa Chadema kuendelea kushikiliwa na magereza licha ya Mahakama kutoa kibali cha kuachiwa kwa dhamana kuwa huko sio kuwaadhibu bali ni kuwapa upako mkubwa wa kisiasa mbele ya wananchi.


Lissu ametoa kauli hiyo jioni ya leo Machi 30, 2018 kupitia ukurasa wake maalumu wa kijamii ikiwa imepita siku moja tokea Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu Wilbard Mashauri kutoa uamuzi wa dhamana ya Mbowe na wenzake licha ya kuwa hawajafikishwa Mahakamani hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa gari walikuwa wamepanda limeharibika.

"Ni ajabu iliyoje kwamba katika wiki ya Pasaka ambayo Yesu Kristo alitiwa kifungoni na baadae kuuawa msalabani, wakaamua viongozi wote wa juu CHADEMA wakamatwe kama alivyokamatwa Yesu Kristo na washtakiwe kama alivyoshtakiwa Yesu Kristo na wasulubiwe kwa kuwekwa mahabusu kama alivyosulubiwa Yesu Kristo msalabani. Hakimu Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi ya Mwenyekiti Mbowe na wenzake, amesema wanastahili kupata dhamana na amewapa lakini Polisi wakaamua kutokuwaachia na kuwalazimisha kuwa kifungoni wakati huu wa Pasaka",amesema Lissu. 

Pamoja na hayo, Lissu ameendelea kwa kusema "wanafanya hivyo kwa kufikiria kwamba wanawakomesha, hawajui watendalo na Mungu awasamehe pamoja na waliowatuma. Kuendelea kuwafunga watu ambao Mahakama imesema wapewe dhamana sio kuwaadhibu, bali ni kuwapa upako mkubwa wa kisiasa mbele ya wananchi. Ni kuwafanya wahanga wa ukombozi wa pili wa nchi yetu".

Tundu Lissu bado yupo nchini Beljium mpaka hivi sasa kwa lengo la kupatiwa matibabu zaidi kutokana na shambulio alilofanyiwa Septemba 7, 2017 la kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa mjini Dodoma na kisha baadae kupelekwa nchini Kenya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527