POLEPOLE : SERIKALI ITAWASHUGHULIKIA WOTE WALIOHUSIKA KUKWAMISHA MIRADI YA MAJI KIGOMA


Katibu wa  itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM taifa Humphrey Polepole amewaahidi wananchi wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kuwa Serikali inayoongozwa na chama tawala itawashughulikia wale wote waliohusika kukwamisha miradi ya maji kutokamilika kwa wakati.

Akizungumza jana Wilayani humo katika Kijiji cha Nyagwijima wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya Maendeleo na utekelezaji wa ilani ya CCM Polepole alisema wilaya hiyo miradi ya maji iliyojengwa ina changamoto na baadhi haijawahi kutoa maji tangu imekabidhiwa kwa halmashauri hiyo na kuwa amefika katika miradi hiyo na kujiridhisha na changamoto hizo.

Polepole alisema wapo baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali walioshiriki kufanya ufisadi watachukuliwa hatua ili kuhakikisha fedha za serikali zinatumika katika miradi iliyokusudiwa.

 Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaagiza wataalamu kutoka mkoani kwenda kutatua changamoto zilizojitokeza ili waendelee kupata maji.

"Nimekuja kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa wa Kigoma inaendelea kwa kasi ile ambayo rais wetu anataka ifanyike na wananchi waweze kuepukana na changamoto hizo, lakini Kakonko kuna changamoto ya miradi ya maji ina changamoto na ni kweli changamoto hizo nimejionea mwenyewe kiasi cha fedha kilichotumika na hata Mbunge kama mwakilishi wa wananchi ameshindwa kufuatilia suala hili",alisema.

 "Hili ni jambo ambalo hatuhitaji kulifumbia macho, tuweke pembeni maneno tufanye kazi kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na tunatatua changamoto zao", alisema Polepole.

Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli anatoa fedha za miradi ili kuwasaidia wananchi waweze kupata maendeleo na miradi itekelezwe kwa wakati hivyo serikali haitawafumbia macho wale wote waliohusika kufanya ufisadi katika miradi hiyo ya maji na wananchi waendelee kuwa wavumilivu watakamilisha miradi hiyo.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliahidi kufuatilia mirafi hiyo na kama kuna waliohusika kuhujumu fedha hizo na kusababisha wananchi kushindwa kupata maji na kuendelea kiteseka.

Alisema miradi ya maji mingi imekabidhiwa kutoka katika Halmashauri ya Kibondo, na mirafi yenye shida ni miradi ya Muhange, Katanga na Nyagwijima ambapo katika mirafi hiyo wananchi hawajawahi kupata maji na mirafi hiyo imejengwa chini ya kiwango na fedha zote zimekwisha kulipwa lakini utekelezwaji hakuna.

Nae mwenyekiti wa bodi ya maji katika Mradi wa Nyagwijima Mathias Yahaya alisema mrafi huo ulitumia zaidi ya milioni 350 hadi kukamilika lakini tangu mradi huo ukamilike umetoa maji katika magati matatu kati ya Magati 17 yaliyojegwa katika mradi huo na mpaka sasa miradi hiyo haitoi maji tena kutokana na kujengwa kwa ubovu na kutozingatia kanuni za ufundi.

Alisema wananchi hao wanaendelea kuteseka na hawana maeneo ya kuchotea maji na kuiomba serikali kuendelea kifuatilia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na wananchi waweze kuendelea kuwa na imani na serikali yao na kuendelea kuchapa kazi.

Aidha katika ziara yake wilayani Kakonko Polepole alishirikiana na wananchi katika uchimbaji wa mtaro wa ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Bukiliro na umwagaji zege katika shule ya sekondari ya Gwanumpu na kutembelea miradi ya maji pamoja na kufanya kikao cha halmashauri kuu ya wilaya.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527