MWOMBEKI STAMBULI AFANYA ZIARA SHINYANGA,ASHIRIKI ZOEZI LA KUFYATUA MATOFALI SHULE YA SEKONDARI NDALA

Mjumbe wa mkutano mkuu UVCCM taifa mkoa wa Shinyanga Mwombeki Stambuli amefanya ziara katika kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga kwa kuitemblea shule ya sekondari Ndala na kuongoza zoezi la ufyatuaji matofali zaidi ya 200 kwa ajili ya ujenzi wa choo katika shule hiyo.

Akiongea na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi jana wakati wa ziara yake, Stambuli alisema ameguswa na tatizo la upungufu wa vyoo katika shule hiyo hali iliyomsukuma kufika shuleni hapo na kuongoza zoezi la kufyatua matofali kwa lengo la kuboresha miundombinu katika shule hiyo.

Alisema hali itawasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo huku akisistiza hatua hiyo ni njia ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli kuboresha sekta mbalimbali.

“Vijana inatakiwa tujitoe na kuwajibika kwa jamii yetu sisi vijana ndiyo tunalea jamii hivyo lazima vijana tuingie kufanya kazi tunapoamua kuandaa utaratibu huu kwa ajili ya kufanya kazi kwa ajili ya wanafunzi wenzetu licha kwamba sisi hatusomi hapa lakini tukiwasaidia wenzetu hawa wao watatusaidia baadae” ,alisema Stambuli.

Kwa upande wake mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya sekondari ya Ndala Brand Kajem alikiri kuwa shule hiyo ina upungufu mkubwa wa mashimo ya vyoo hali inayochangia wanafunzi kuchelewa masomo kutokana foleni wanapokwenda chooni kujisaidia hasa wakati wa mapumziko na kuhatarisha afya zao.

“Changamoto ya vyoo ni kubwa tangu shule hii ianzishwe ina matundu manne tu ya vyoo na matundu hayo manne kwa utaratibu tulitakiwa tuwe na wanafunzi 90 lakini idadi ya wanafunzi tulionao ni zaidi ya 350 kwa mantiki hiyo niwaombe wadau kuunganisha nguvu ya pamoja kutatua changamoto hiyo na tusitegemee serikali pekee”, alisema Kajem. 

Ziara hiyo pia ilihusisha viongozi CCM kata ya Ndala akiwemo mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Shinyanga na aliyekuwa mgombea wa kiti cha udiwani kata ndala Abel Joel Kaholwa ambaye aliwaomba vijana kuunga mkono jitihada zinazotekelezwa na Chama Cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo katika taifa bila kujali itikadi za vyama. 

Stambuli anafanya ziara katika mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuimarisha jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM na kuongeza hali ya utendaji kazi kwa vijana kutambua uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kutambua dhamira kubwa aliyonayo Raisi wa Jamuhuri ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli juu ya utendaji kazi.
Wa kwanza kushoto ni Mjumbe wa mkutano mkuu UVCCM mkoa wa Shinyanga Mwombeki Stambuli  akiwa na akiwa na Mwenyekiti wa CCM kata ya Ndala bi.Magreth John Lukaka wakifyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa choo katika shule ya sekondari Ndala - Picha zote na Steve Kanyefu - Malunde1 blog
Mjumbe wa mkutano mkuu wa UVCCM mkoa wa Shinyanga Abel Joel Kaholwe akiweka mchanga katika mashine ya kufyatulia tofali.
Umoja ni nguvu ,wanaCCM kata ya Ndala wakishirikiana katika zoezi la ufyatuaji tofali kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule ya Sekondari Ndala
Stambuli akisisitiza jambo mbele ya wanaCCM na kuwataka vijana kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuendekeza starehe na kuwajibika ipasavyo ili kulijenga taifa la vijana wenye maendeleo
WanaCCM kata ya Ndala wakimsikiliza Stambuli.
Katika ziara hiyo pia kulifanyika Bonanza la michezo ambapo Stambuli alitoa seti moja ya jezi kwa timu ya vijana kata ya Ndala na hapa akisalimiana na vijana kabla ya kuanza kwa bonanza hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527