MAPYA YAIBUKA SAKATA NA MUUGUZI KUPIGWA NGUMI ZA USO SHINYANGA..DIWANI AFUNGUKA KILA KITU (Video)


Diwani wa kata ya Bunambiu Richard Sangisangi (CCM).

Sakata la Muuguzi wa kituo cha afya Bunambiu kilichopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Hilda Simon (35) kudaiwa kupigwa ngumi usoni na kifuani na diwani wa kata hiyo Richard Sangisangi (CCM) limechukua sura mpya baada ya diwani huyo kuibuka na kusema hakumpiga muuguzi huyo. 

Leo Alhamis Machi 15,2018 Sangisangi amefika katika ofisi ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa taarifa zilizotolewa kuwa Machi 8,2018 alimpiga muuguzi wa kituo cha Bunambiu siyo za kweli. 

Alisema siku hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa kuna mgonjwa hahudumiwi vizuri alifika katika kituo cha afya kuona kuna nini kinaendelea akakuta mgonjwa ana hali mbaya ndipo akamfuata muuguzi Hilda kumuuliza kulikoni ndipo muuguzi huyo akamtaka diwani aondoke kituoni hapo akidai hajaajiriwa na diwani. 

“Kufuatia hali ndipo nikamwambia huyo muuguzi aondoke aje nesi mwingine aliyetambua tatizo la mgonjwa amwandikie rufaa,hakutaka kutoka ,nikamfuata nesi aliyetambua mgonjwa hana damu,nikamleta kisha kumwambia Hilda pisha,alipokataa kutoka ndipo nikamshika mkono nikamsogeza pembeni na nesi mwingine akaendelea kuhudumia”,alieleza Sangisangi. 

“Mimi sikumpigana siwezi kupiga..nasema siyo kweli,mimi najitambua kama kiongozi,nina dhamana ya kuongoza watu,nina dhamana ya kusimamia watu..kama nitaonekana nina makosa sheria ichukue tu mkondo wake..mimi nipo tayari kwa lolote”,aliongeza Sangisangi. 

MTAZAME HAPA SANGISANGI AKIZUNGUMZIA TUKIO LA KUDAIWA KUMPIGA MUUGUZI


Machi 9,2018 Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kusema jeshi hilo linamshikilia diwani Richard Sangisangi (48) kwa kumshambulia kwa kumpiga ngumi usoni na kifuani muuguzi wa kituo cha afya Bunambiu Hilda Simon (35). 

Kamanda Haule alisema Sangisangi alimpiga muuguzi huyo katika kituo cha afya Bunambiu na kumsababishia maumivu makali. 

Alisema chanzo cha tukio hilo lililotokea Machi 8,2018 majira ya saa tatu na nusu asubuhi ni diwani huyo kutokuwa na imani na muuguzi huyo wakati akiwahudumia wagonjwa hivyo kuamua kumshambulia kwa kumpiga ngumi. 

“Mtuhumiwa tumemkamata na tutamfikisha mahakamani mara tu baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika,natoa wito kwa wananchi na viongozi kuacha kujichukulia sheria mkononi”,alisema kamanda Haule. 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,waliiambia Malunde1 blog kuwa diwani huyo alimtuhumu muuguzi huyo kuwa hahudumii wagonjwa vizuri na kumtaka aondoke kituoni na alipogoma ndipo diwani alipoamua kumshambulia mbele ya wagonjwa. 

Walisema diwani huyo alipigiwa simu na wananchi wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika kituo hicho cha afya hapatiwi huduma vizuri na ndipo diwani huyo alipoomba kuongea kwa simu na muuguzi wa zamu,muuguzi akamsihi diwani afike kituoni na alipofika akaanza kumshambulia muuguzi huyo. 

“Huyu diwani alipigiwa simu na ndugu wa mgonjwa,kwamba mgonjwa wao hapatiwi huduma vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”,walieleza. 

Hata hivyo habari zaidi zinasema,wakati Hilda Simon akiendelea kuhudumia wagonjwa,ghafla muuguzi mwingine ambaye hakuwa zamu aliingia katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa mgonjwa huyo kuwa ndugu yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga. 

“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa mgonjwa wakaamua kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na nesi wa zamu,nesi akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza kuonesha ubabe kwa kumshambulia muuguzi ambaye alikuwa zamu na alikuwa anasimamia kituo cha afya kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo kazini”,walisema mashuhuda wa tukio hilo. 

Tukio hilo lilitokea wakati wanawake wakisherehekea siku ya wanawake duniani. 
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527