MGOMBEA UDIWANI WA CHADEMA AHAMIA CCM SIKU TATU TU BAADA YA UZINDUZI WA KAMPENI


Chadema kimepata pigo baada ya mgombea wake wa udiwani Kata ya Manzase wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma, Mashaka Chalo kujiunga na CCM pamoja na wanachama wengine 131.


Chalo amehama Chadema siku ya tatu tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuzindua kampeni katika Kata hiyo na kunadiwa jukwaani na mbunge wa viti maalum, Kunti Majala.

Uchaguzi wa ubunge jimbo la Siha, Kinondoni na katika Kata 10 nchini utafanyika Februari 17, 2018. Uchaguzi katika Kata hiyo unafanyika baada ya aliyekuwa diwani, Peter Madanya (CCM), kufariki dunia mwishoni mwa mwaka jana.


Mgombea huyo amehamia CCM jana Februari 4, 2018 katika kijiji cha Manzase wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho na kupokewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo.


Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amesema uamuzi wa Chalo kujiuzulu ni ushindi kwa chama tawala.


“Mpogolo unaweza kufungua kampeni hizi na kisha kuzifunga maana kazi imekwisha. Tulikuwa na wagombea watatu, lakini kuondoka kwa huyu, CCM tunaona kazi imekwisha. Wagombea wengine waliobaki hata tukilala usingizi hakuna kitu ushindi ni wetu,” amesema.


Mgombea wa CCM katika Kata hiyo ni Amosi Mloha.


Lusinde amesema Chadema walimpitisha Chalo dakika za mwisho kuwania udiwani bila kujua kuwa alikuwa pandikizi la CCM.


Akizungumza katika mkutano huo Chalo amesema amerejea CCM kwa sababu ni chama chake na kimemlea.

Na Habel Chidawali,Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527