MEYA AKATAA GARI LA KUTEMBELEA ANUNUA GARI LA KUSOMBEA TAKA


Uamuzi wa Meya wa Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Willy Mbogo wa kukataa kununuliwa gari la kutembelea umewanufaisha wananchi baada ya fedha zilizotengwa kiasi cha zaidi ya shilingi   milioni 150 kwa ajiri ya kununua gari lake kutembelea na kuamua  nunua gari la kusombea takataka.

Awali Manispaa hiyo ilitenga kiasi cha Tshs 159,000,000/= kwa ajiri ya gari la Meya ,lakini meya wa Manispaa hiyo Willy Mbogo alikataa na kueleleza fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo kwa kununua gari la kusombea taka .

Gari hilo lori lenye namba za usajiri SM 12244 lenye uwezo wa kubeba tani 16 lilikabidhiwa leo   kwa uongozi wa Manispaa hiyo katika ofisi za Manispaa hiyo zilizoko katika Mtaa wa Ilembo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Matinga.

Akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Deodatus Kangu alieleza kuwa Manispaa hiyo ilikuwa imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajiri ya kununulia gari la kutembelea Meya wa Manispaa hiyo ambaye hana gari la kutembelea kwa ajiri ya shughuli za manispaa hiyo hata hivyo alikataa kununuliwa gari la badala yake alielekeza fedha hizo zitumike kununua gari la kusombea taka.

Kangu alieleza kuwa fedha hizo zilizokuwa zimetengwa kutokana na makusanyo ya mapato ya ndani yaliyopatikana katika mwaka wa fedha wa mwaka 2017 na 2018.

Alisema wakazi wa manispaa ya Mpanda huzalisha kiasi cha tani 70.5 za taka ngumu kwa siku sawa na tani 25,732.5 kwa mwaka ambapo asilimia kubwa ya taka hizo ni taka toka majumbani na maeneo ya biashara.

Kaimu Mkurugenzi Kangu alifafanua kuwa kutokana na upatikanaji wa lori lenye uwezo wa kubeba tani 16 litasaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa tatizo la mrundikano wa taka ngumu zilizokuwa zinabaki kwenye viziba au kwenye maeneo yaliyoandaliwa kwa muda mrefu.

Alizitaja baadhi ya changamoto zilizopo katika katika utekelezaji wa udhibiti wa taka ngumu katika Manispaa ya Mpanda kuwa ni upungufu na uchakavu wa malori ya kuzoa taka na kusafirisha taka ngumu .

Changamoto nyingine ni ongezeko la idadi ya wakazi inayopelekea ongezeko la uzalishaji wa taka ngumu na ukosefu wa dampo la kisasa kwa ajiri ya uchambuzi na uzikaji wa taka ngumu .

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga aliitaka Manispaa hiyo kuhakikisha gari hilo linatumika kwa makusudio yake na lisitumike kwa matumizi tofauti na yalivyokusudiwa .

Aliitaka manispaa hiyo kulitunza gari hilo la kulifanyia matengenezo kila yatakapo hitajika na waakikishe gari hilo muda wote linakuwa safi siyo kwa kuwa gari hilo ni la kusombea taka basi waliache liwe chafu.

Pia aliishauri halmashauri hiyo isiishie kununua gari hilo tu kwani mahitaji ya gari la kusombea taka bado yanahitajika kutokana na jinsi manispaa hiyo inavyokuwa kwa kasi kubwa.

Haidari Sumry Diwani wa Kata ya Makanyagio alimpongeza Meya wa Manispaa hiyo kwa uamuzi wake huo wa kizalendo aliuchukua kwa manufaa ya wakazi wa manispaa na mkoa kwa ujumla.

Alisema jambo hilo la kubadili matumizi ya fedha zilizokuwa zimetengwa kununulia gari lale ni jambo la kuigwa kwa viongozi wengine.

Nae Meya wa Manispaa ya Mpanda Willy Mbogo alisema uamuzi huo aliamua kuutoa sio kwa manufaa yake binafsi bali alitanguliza maslahi ya wananchi kwanza na amewaomba wananchi kuwaunga mkono pindi Manispaa hiyo wanapokuwa wanataka kuongeza kipata cha Halmashauri hiyo.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda Deodatus  Kangu akisoma taarifa fupi wakati wa mapokezi ya lori tani 16 kwa ajiri ya uzoaji wa taka ngumu katika manispaa ya Mpanda.-Picha na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga akimkabidhi meya wa manispaa ya Mpanda Willy Mbogo funguo ya gari lori litakalotumika kwa ajiri ya usombaji wa taka.
Meya wa manispaa ya Mpanda Willy Mbogo akimkabidhi funguo za gari lori lenye namba SM 12244 Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda Deodadus Kangu.Picha na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527