MAHAKAMA NCHINI KUANZA KUSIKILIZA KESI KWA NJIA YA MTANDAO


WAKATI mahakama nchini zinatarajia kuanza kusikiliza kesi kwa kutumia mtandao kuanzia mwakani, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza gharama.

Waziri Kabudi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam  wakati akihojiwa na waandishi wa habari, baada ya kufungua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na kuongeza kuwa mashahidi watatoa ushahidi wakiwa nje ya mahakama.

Waandishi wa habari walitaka kupata maoni yake kuhusiana na mpango wa mahakama wa kufanya maboresho kwa kuanza kusikiliza kesi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Mimi mwenyewe sikujua kabisa matumizi ya mtandao hata WhatsApp, nimeanza kutumia hivi karibuni baada ya kuapishwa…  teknolojia yoyote mpya inapokuja ambao ni wagumu kuielewa ni watu wa umri wangu, lakini kwa vijana wanaelewa kwa haraka zaidi,” alisema.

Waziri alisema kuwa utaratibu huo wa mahakama kuingia kwenye mfumo wa Tehama utasaidia kupunguza gharama kwa mfano, kesi ikiwa Dar es Salaam na shahidi yupo Mbeya hatalazimika kusafiri kwa ajili ya kutoa ushahidi.

“Haitatakiwa kutolewa mkoani Mbeya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya ushahidi, atatoa ushahidi wake akiwa Mbeya na jaji ama hakimu ambaye yupo Dar es Salaam atamuona na kumsikiliza,” alisema.

Aliongezea: “Hata kwa maabusu ambao wapo gerezani kwa ajili ya kwenda kuahirisha kesi au maombi ya dhamana hana haja tena ya kwenda mahakamani.”

Hata hivyo, Prof. Kabudi alieleza kuwa kuna haja ya watu kujifunza.  Ni kweli tunahitaji kujifunza zaidi kuhusu matumizi ya mtandao, lakini umuhimu huo ni kwa watu wenye umri mkubwa kuliko vijana, maana vijana mtandao anao mkononi,” alisema. Kabudi alisema teknolojia kwa sasa imesogezwa hadi kwenye simu kwa hiyo mtu anaweza kupata taarifa zake za kesi.

Alisema baada ya muda Watanzania wengi watafurahia mfumo wa mahakama kwa njia ya Tehama kwa kuwa kwa sasa miundombinu ipo pamoja na uelewa, ingawa ni jukumu ya mahakama kuwaelimisha wananchi kuhusiana na utaratibu huo.

Alisema suala hilo ni muhimu na linaendana na wakati, hivyo ni jambo nzuri kuipongeza mahakama kwani mahakama zinakuwa nyuma kwenye mabadiliko, lakini kwa Mahakama ya Tanzania imekuwa mbele ya taasisi nyingi za sheria katika kuleta mabadiliko.

Aidha, aliwataka wananchi wa Kigamboni waitumie mahakama hiyo na kuyatunza majengo hayo ili ya yadumu kwa muda mrefu.

ONYO WASIMAMIZI MIRATHI Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi aliwataka wasimamizi wa mirathi kutojihusisha na mali za urithi na kwamba kazi yao ni kuhakikisha mali zinawafikia wahusika badala ya kujinufaisha.

Waziri Kabudi alisema msimamizi wa mirathi sio mrithi wa mali, kazi yake ni kugawa mali kwa wahusika halali, lakini wengi wao wamekuwa wakijisahau.

”Huyu msimamizi anatakiwa kutoa taarifa mahakamani baada ya miezi sita toka alipoteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi, wengi huwa hawafanyi hivyo na matokeo yake kujiona wao ndio warithi wa mali, nataka wajue kuwa msimamizi wa mirathi  sio mrithi wa mali,” alisisitiza.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.