KIONGOZI WA CHADEMA AFARIKI KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA...MBOWE AFUNGUKA


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akionyesha mbele ya waandishi wa habari picha ya kiongozi wa chama hicho Kata ya Hananasif, Daniel John akisema alipatikana akiwa amekufa baada ya kutoweka jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis. 
***

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kiongozi wa chama hicho katika Kata ya Hananasif, Daniel John amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Mbowe akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13,2018 amesema John alitoweka siku moja iliyopita.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hana taarifa hizo lakini anawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Amesema baada ya mawasiliano atatoa ufafanuzi kesho Februari 14,2018.

Mbowe amesema John ambaye ni katibu kata alitoweka akiwa na Reginald Mallya ambaye alijikuta yupo ufukweni mwa bahari.

Mbowe amesema walitoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa John na kwamba, walipokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walielezwa kuna mwili ulipelekwa na polisi.

Amesema mwili huo ulitambuliwa na mkewe John na una michubuko inayoashiria alikabwa, una jeraha la panga kichwani na upande mmoja wa kichwa umebonyea kuashiria alipigwa na kitu kizito.

Kuhusu Mallya amesema alipigwa panga kichwani na alivunjwa mkono. Mbowe ametaka polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Mallya aliyekuwapo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari amesema walikuwa wakitembea na John ndipo waliposimamishwa na kuingizwa ndani ya gari.

Amedai alipigwa hadi kupoteza fahamu na alipozinduka alijikuta ufukweni alikojikokota hadi barabarani ambako alipata msaada wa bajaji na alikwenda Hospitali ya Mwananyamala alikotakiwa kuwa na taarifa ya polisi ambayo aliipata Kituo cha Polisi Oysterbay.

Na Kalunde Jamal na Pamela Chilongola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527