LHRC,TLS NA THRDC KUFUNGUA KESI DHIDI YA SHERIA ZINAZOUMIZA TANZANIA

TAASISI tatu zinazojihusisha na utetezi wa sheria na haki za binadamu, zitafungua jumla ya kesi 10 ndani ya miezi mitatu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kupinga zilichodai sheria kandamizi zinazominya demokrasia na uhuru wa kujieleza.


Taasisi hizo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).


Baadhi ya sheria ambazo zimeanza kupambana nazo kwa kufungua kesi ili zifanyiwe marekebisho, zimesema, ni Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Uchaguzi.


Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, viongozi wa taasisi hizo walisema tayari wameshafungua kesi mbili katika Mahakama Kuu na kwamba kesi nane zitafunguliwa baada ya miezi miwili.


Walisema kesi hizo zimefunguliwa na wapiga kura wawili, Bob Chacha Wangwe na Allan Bhujo watakaowakilishwa na mawakili kutoka taasisi hizo tatu.


"Tayari tumeshafungua kesi mbili katika mahakama kuu, na kesi zingine nane tutazifungua miezi miwili ijayo na kufanya jumla ya kesi kuwa 10," alisema Fatma Karume kutoka TLS.


Akizungumza katika mkutano huo, Karume alisema wamejiandaa kuzipinga sheria hizo alizoziita kandamizi, kwa mustakabali wa Watanzania.


"Hatutakata tamaa kwenye hili," alisema Karume. "Tumeshuhudia vitendo vingi ndani ya nchi vinavyowanyima wananchi demokrasia na uhuru wa kujieleza.


"Hii ni kinyume na katiba na ndiyo maana tumeunganika kupinga sheria hizo kwa mustakabali wa taifa."


Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Anna Henga, alisema haki ya kukusanyika, kujieleza ni haki ya kila Mtanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527