WAZIRI WA MADINI ASAINI KANUNI ZA SHERIA MPYA YA MADINI



Waziri wa Madini Angellah  Kairuki amesaini Kanuni za Sheria Mpya ya Madini ambapo  Wakala wa Jiolojia Nchini (GST) amepewa nguvu ya kisheria ya kuingia katika ardhi yoyote kufanya utafiti wa kina wa madini.
Mwaka jana Bunge lilipitisha Sheria mbili za madini ambazo zinalenga  kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Madini.
Hata hivyo kanuni za sheria hizo zilikuwa bado hazijasainiwa na Waziri wa Madini hadi Januari mwaka huu jambo ambalo lilimkera Rais John Magufuli na kutoa agizo zikamilike  ndani siku tano.
Akizungumza leo Januari 28  Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema kuwa kanuni hizo zimesainiwa  Januari 9 mwaka huu ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kuagiza kukamilishwa kwa mchakato wa kanuni hizo ndani ya siku tano.
Biteko alikuwa akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ilitembelea ofisi za GST mjini Dodoma.
“Kuna watu wanasema sheria hii mpya itafukuza wawekezaji na hakuna wawekezaji wapya watakaokuja lakini nataka kuwaambia kuwa kuna wageni wengi wanakuja kutaka kuwekeza katika migodi mikubwa,” amesema.
Amesema  wastani katika kila wiki wamekuwa wakipokea wawekezaji kati ya 10 na 20 ambao wanaonyesha nia ya kuwekeza nchini katika sekta hiyo kwa hiyo sheria sio kikwazo kwao.
Alisema kujitokeza kwa wingi kwa wawekezaji kunatokana na sheria hiyo  kuweka uwazi katika taratibu na kanuni za kuwekeza.
Biteko amesema  lengo la wizara yake ni kuongeza uchangiaji wa sekta ya madini katika pato la taifa kutoka asilimia 4.8 ya mwaka jana hadi kufikia asilimia 10 kama Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano unavyosema.
Tafiti zifanywe na GST
Wakichangia kwa nyakati tofauti wabunge wamesema ili kuifanya sekta hiyo kuwa na manufaa zaidi ni vyema Serikali ikaacha suala la utafiti wa kina ukafanywa na GST.
Mbunge wa Tarime vijijini (Chadema) John Heche amesema kampuni kubwa zinazokuja nchini kwa ajili ya uwekezaji katika sekta hiyo, yanafanya utafiti kwa kipindi kirefu sana huku Serikali ikiwa hainufaiki.
“Wengine wanakuja kufanya utafiti kwa zaidi ya miaka 10 na bado wakiondoka wanasema hawajapata kitu. Sisi tuna watu wetu hapa (GST) wapewe mamlaka ya kisheria ya kufanya Exploration (utafiti wa kina) na wawekezaji wanapokuja wapewe leseni za uchimbaji,” amesema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Ngalawa (Ludewa-CCM) ambaye amesema kuwapa GST jukumu la kufanya utafiti wa kina kutaongeza mapato kwa sababu wawekezaji watakapokuja kuwekeza watalipia gharama za utafiti huo.
 “Unakuta wengine wanakuja kufanya utafiti miaka mitatu ama na zaidi hakuna wanalotufanyia,”alisema Ngalawa ambaye alikuwa ndio mwenyekiti wa kikao hicho.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM) Desdurius Mipata alitaka kamati hiyo kufahamishwa kuhusiana na utajiri wa nchi katika sekta ya madini kutokana na tafiti zilizofanywa na GST.
“Tuko matajiri kiasi gani? Tunakilinganishwa na akinani? Kwa kiasi gani naomba nipewe majibu hata kama sio leo,”amesema.
Gharama kubwa za vibali
Mkurugenzi wa idara ya Kanzidata wa GST, Yokbeth Myumbilwa alisema miongoni mwa changamoto ya wakala huo ni kulazimika kulipia vibali kila siku kwa watafiti wanapofanya tafiti zao mbugani.

“Tunalazimika kulipia vibali kila siku hata kwa vibarua wakati tunapofanya tafiti katika maeneo ya mbugani (hifadhi),”alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Joyce Sokombi ameshauri wizara hiyo kulifanyia kazi tatizo hilo ili kuwawezesha wataalam wa wizara hiyo kutimiza majukumu yao kwa urahisi.

Elimu ya majanga ya asili itolewe

Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema) Willfred Lwakatare alishauri GST kutoa elimu juu ya kujikinga na majanga ya asili yakiwemo matetemeko kwa kutumia lugha rahisi.

“Mkoa wa Kagera mpeleke pia monitoring center (vituo vya uangalizi) ili waweze kupata taarifa.  Kuna vitetemeko vidogovidogo vimekuwa vikitokea vinazua hofu,” amesema.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527