WAANDISHI WA HABARI WAPANDISHWA KORTINI KWA KUJIFANYA USALAMA WA TAIFA,KUTAPELI SANGOMA


Waandishi wa habari watano wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamefikishwa mahakamani wilayani Kahama kwa makosa ya kujifanya maafisa usalama wa taifa kutoka ikulu na kujipatia fedha shilingi Milioni 1 kutoka kwa mganga wa jadi Jane Mbeshi (46).

Waandishi wa habari wanne kati ya watano ambao ni Paul Kayanda wa gazeti la Uhuru,Raymond Mihayo- Habarileo,Shaban Njia – Jamboleo,Simon Dioniz – Radio Kwizera wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kahama leo Jumatano Januari 10,2018 nana George Maziku ambaye hajulikani anaandikia chombo gani anatafutwa.

Akisoma mashtaka mahakamani hapo leo asubuhi,Hakimu Kazi wa mahakama ya wilaya ya Kahama,Keneth Mutembei alisema washtakiwa hao walijifanya maafisa wa usalama wa taifa kutoka Dar es salaam,Kigoma,Kagera,Shinyanga na Kahama kisha kujipatia shilingi 1,000,000/- kutoka kwa mganga wa jadi Jane Mbeshi (46) mkazi wa kitongoji cha Ng’wande kata ya Mwaluguli wilayani Kahama baada ya kumtishia kuwa anapiga ramli chonganishi.

Alisema waandishi wa habari watatu ambao ni Paul Kayanda,Shaban Njia na Dioniz Maziku walikamatwa jana Januari 9,2018 saa saba na nusu mchana na jeshi la polisi wakijifanya maafisa wa usalama wa taifa na kujipatia fedha kutoka kwa mganga wa jadi Jane Mbeshi.

Hakimu huyo alisema walikamatwa baada ya kuwekewa mtego kwani waliahidiwa fedha zingine tena shilingi milioni 1,000,000/- na mganga huyo wa jadi ambaye pia ni mkandarasi baada ya kuchukua shilingi milioni 1 tarehe 6.1.2018 wakiwa na waandishi wa habari wengine ambao ni Raymond Mihayo aliyekamatwa jana usiku saa nne akiwa nyumbani kwake,na George Maziku ambaye bado anatafutwa kutokana na kutojulikana alipo.

Mara baada ya kusoma mashtaka hayo,hakimu huyo alisema dhamana ipo wazi kwa washtakiwa ambapo walikana mashtaka hayo walikana kutenda makosa hayo.

Washtakiwa walirudishwa gerezani baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Na Karim Mtilah

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527