RAIS MAGUFULI ATOA SIKU TANO KWA MAWAZIRI WAWILI


Rais John Magufuli amemuapisha Doto Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini na kuiagiza wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kanuni za sheria mpya ya madini namba 7 ya mwaka 2017 inasainiwa ifikapo Ijumaa, Januari 12, 2018.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya Biteko kuapishwa leo Jumatatu Ikulu jijini Dar es Salaam na ameelezea kutoridhishwa kwake na namna viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole na bila kujali maslahi ya nchi.

“Sheria hii imepitishwa na Bunge na mimi nikaisaini tangu mwezi wa saba mwaka 2017, mpaka leo ni miezi saba bado hamjasaini kanuni zake ili sheria ianze kutekelezwa, na wahusika wote wapo, yaani mpaka leo hamjaelewa Watanzania wanataka nini? Amehoji Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527