RAIS MAGUFULI AMTUMBUA MKURUGENZI WA BUTIAMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli leo Januari 23, 2018 ametengua uteuzi wa Mkurgenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Butiama, Solomoni Kamlule Ngiliule kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yake kama ilivyopaswa.



Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo akizungumza na waaandishi wa habari,ametangaza uamuzi huo leo, zikiwa zimepita siku tatu tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa maagizo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.


“Kutokana na hali iliyojitokeza Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli ambaye pia ndiye Waziri mweye dhamana wa Ofisi ya TAMISEMI, amechukua fursa hiyo baada ya yaliyojiri Mkoa wa Mara, hasa katika Halmashauri ya Butiama, Amemtengua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Butihama, Ndugu Solomoni Kamnule Ngiriule, kuanzia leo hii kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yake kama mkurugenzi mwenye dhamana,” amesema Waziri Jafo.


Waziri Jafo amemtaka Katibu wa TAMISEMI kuchukua hatua dhidi ya mweka hazina aliyekuwapo kipindi ambacho ubadhirifu huo ulipotokea.


“Na hata hivyo namuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuchukua hatua stahiki kwa mweka hazina wa Halmashauri ya Butihama ambaye alikuwepo kipindi hicho ubadhirifu ulipokuwa unatokea,” amesema Waziri Jafo.


Kufuatia hatua hiyo, Waziri Jafo amewataka watendaji wote wa Wizara yake kuhakikisha kuwa wanatimiza majukumu yao ipasavyo, kwani walipewa jukumu la kuwatumikia wananchi na siyo jambo jingine.


“Hata hivyo niwatake watendaji wote wa TAMISEMI kuhakikiha kwamba wanatimiza wajibu wao kwa dhamana kubwa waliyopewa kwa ajili ya kuwatumikia watanzania,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527