JESHI LA POLISI LATOA MAJIBU KWA WAZIRI BAADA YA AGIZO LA KUWAKAMATA WATUHUMIWA WA UJANGILI NDANI YA SIKU SABA

Jeshi la Polisi limesema limepokea agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla la kuwachukulia hatua watu wanne ndani ya siku saba kwa madai wanashiriki katika mtandao wa ujangili, lakini halifanyi kazi kwa shinikizo.

Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa amesema polisi wanafanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za Jeshi hilo.

Juzi, Kigwangalla mbali na kutoa agizo hilo, amesema watu hao wanne pia walipanga njama za kumuua mwanaharakati, Wayne Lotter na kwamba polisi wakishindwa kuwakamata atawashtaki kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwakalukwa amesema jukumu lao ni kukamata wanapopata shitaka la kuwapo kwa kitu kisicho cha kawaida, kuchunguza na kupeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine.

“Kazi yetu ni kukamata, kuchunguza na kupeleka kwa DPP kwa ajili ya taratibu nyingine, hatufanyi kazi kwa matamko ya bungeni,” amesema na kuongeza;

“Alichokisema mheshimiwa Kigwangalla nimekisoma kwenye vyombo vya habari akihusisha na suala la mwanaharakati aliyeuawa, sisi hatufanyi kazi kwa kufuata vyombo vya habari vimeandika nini au limetolewa tamko gani au kuna shinikizo gani, tunafanya kwa kufuata taratibu zilizopo.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527