CHADEMA KUFANYA KIKAO CHA DHARURA KESHO



Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kesho inakutana katika kikao cha ‘dharura’ jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 12, 2018, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hali ya kisiasa nchini.

Mwananchi lilipotaka kujua kama lengo la kikao hicho ni kujadili ziara ya waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwenda Ikulu, Mwalimu amesema kikao hicho si cha dharura kwani kilipangwa kufanyika Desemba mwaka jana lakini kiliahirishwa kutokana na sikukuu za mwisho wa mwaka.

Amesema ajenda za kikao hicho zilipangwa kabla Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema hajaenda Ikulu hivyo hakika uhusiano na ziara hiyo ila huenda jambo hilo likajitokeza.

“Suala hilo halipo kwenye ajenda ila linaweza kujitokeza na likijitokeza litazungumziwa lisipojitokeza basi,” amesema Mwalimu na kuongeza;

“Hata hivyo kwa upande wake inaweza kuwa fursa nzuri kuielezea Kamati Kuu na viongozi wenzake nini kilitokea.”

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527