AJIUA KWA HASIRA YA KUKIMBIWA NA MKE


Mwanaume aitwae Anord Msafiri (44) mkazi wa kijiji cha Nkomolo kata ya Nkomolo wilayani Nkasi mkoani Rukwa amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani kutokana na hasira baada ya kukimbiwa na mke wake.

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa kijiji hicho Teddy Chambala alisema kuwa marehemu alijinyonga ndani ya nyumba yake juzi Januari 23,2018 majira ya saa 9 alasiri na majirani walibaini kifo hicho majira ya saa 12 za jioni siku hiyo.

Aliiambia Malunde1 blog kuwa licha ya marehemu huyo kutoacha ujumbe wowote kuhusiana na kifo chake lakini siku chache kabla ya tukio hilo mke wake alitoroka nyumbani kwa madai kuwa amechoka kuishi na mwanaume huyo ambaye ni mlevi na alikuwa akimpiga mara kwa mara.

Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema kuwa mke wa marehemu huyo alitoroka nyumbani na kuwaacha watoto wawili aliozaa na Msafiri kitendo kilichosababisha apate usumbufu wa kuwalea na maisha kuwa magumu.

Alisema kutokana na kitendo hicho ndipo Msafiri alipoamua kujinyonga kutokana na ugumu wa maisha, hasira pamoja na msongo wa mawazo kwani alibaki mpweke akiwalea watoto peke yake. 

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo lakini polisi bado wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527