NYALANDU KUUNGANA NA MAKAMANDA WA CHADEMA KWENYE KAMPENI ZA UCHAGUZI WA UDIWANI

Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu leo ataungana na viongozi wa Chadema kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika katika kata 43 nchi.


Akizungumza jana Novemba 11, kwenye ufunguzi wa kampeni hizo Kimara Suka jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema amempokea Nyalandu na ataungana naye kwenye mkutano mwingine kama huo utakaofanyika Mtwara mjini leo.


‘’Kila anayeondoka chama tawala anaitwa fisadi, potelea mbali wamempokea na wengine wengi watahamia kuleta mabadiliko’’ alisema na kuongeza


"Mabadiliko hayaji ghafla yanakuja taratibu na ujio wao ndiyo mwanzo wa mabadiliko tulipoanza na tulipo sasa kuna tofauti kubwa" amesema Mbowe.


Alifafanua kwamba haungi mkono nchi kuwa na wezi, lakini anashauri sheria iachwe iamue haki badala ya kuingiliwa kama inavyofanyika kwa mahakama.Huku akidai kwamba watawala wana hofu ndiyo maana hawataki ushauri.


Alisema wataendelea kupigania haki ya kupigania haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na ipo siku wataingia mtaani kuidai bila kuogopa vifaru.


Alisema huu siyo wakati wa kuogopa na kukaa kimya ni wakati wa kusimama na kutetea haki ya kufanya siasa.


Kuhusu uchumi kusinyaa alisema ni kweli umesinyaa na inaonekana wazi jinsi maisha yalivyo wananchi, wafanyabiashara, watawala wote wanalia njaa hakuna mwenye nafuu.


Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema anahitaji kuongeza nguvu ya kuleta maendeleo katika manispaa hiyo, hivyo mgombea udiwani kata ya Saranga Ephram Kinyafu anatosha.


Naye Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Frederick Sumaye alihoji kuhusu hali za wananchi kuendelea kuwa mbaya.


"Tumeamua na tunamaanisha wakati huu ushindi ni lazima, na mtakaotupa ushindi ni nyie wananchi" alisema Sumaye.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527