KIGWANGALLA AMTUMBUA MKURUGENZI WA WANYAMAPORI WA HIFADHI YA SERENGETI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dr. Hamis Kigwangalla amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa wanyamapori wa hifadhi ya Serengeti, kwa tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Dr. Kigwangalla ambae alizungumza kutokea ndani ya Hifadhi ya Serengeti, amefanya ziara ya kushtukiza na kuuzunguka mpaka wote wa mashariki hifadhi ya Serengeti inakopakana na Pori Tengefu la Loliondo.

Pori la Loliondo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu ambapo Dkt. Kigwangalla ameagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gaudence Milanzi kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Wanyama Pori, Profesa Alexander Songorwa mara moja ambapo ametaja sababu  3 za kumsimamisha kazi:

1. Tuhuma za kuhujumu Serikali kwa kutoa taarifa za siri za Serikali kwa vyombo vya habari na kutunga taarifa zenye kulenga kuchochea mgogoro wa Loliondo. (Jana usiku zilizunguka taarifa kwamba Dkt. Kigwangalla yupo na msafara wa gari mbili binafsi (private) njiani kwenda Loliondo na kwamba atalala Hotel ya Acacia iliyopo Karatu, leo msafara wake umekuwa ukifuatiliwa na watu wasiojulikana ambapo kila hatua aliyofikia ilikuwa ikiripotiwa kwenye mtandao, hali ambayo imetishia usalama wa kiongozi huyo.

2. Waziri Kigwangalla amesema Mkurugenzi huyo amekuwa akifanya kazi kwa maelekezo ya muwekezaji wa Kampuni ya Utalii wa Uwindaji ya OBC (maarufu kama kampuni ya kiwindaji ya Wafalme wa Dubai). Kampuni hii imekuwa ikihusishwa na kashfa kwa miaka zaidi ya 26.

3. Aidha Prof. Songorwa amekuwa akihusishwa na kashfa ya kushiriki kugawa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria ambapo wiki mbili zilizopita Waziri Kigwangalla alisitisha mchakato wa kuhuisha leseni za uwindaji uliofanywa na Prof. Jumanne Maghembe, aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii kwa tuhuma za rushwa na kukosekana uwazi kwenye mchakato huo ambapo sasa ameelekeza mchakato wa kugawa vitalu ufanywe kwa njia ya mnada.

Pia, ameelekeza TAKUKURU kuanza kuchunguza kashfa za rushwa dhidi ya kampuni ya OBC na waanze kwa kumhoji Mollel (Mkurugenzi wa OBC) ambae amekuwa akijigamba kila kona kuwa “nilimhonga Maghembe dola 200,000, huyu kijana Kigwangalla dola 100,000 inamtosha” 

Dkt. Kigwangalla amesisitiza haongeki na ndiyo maana jitihada za Mollel kumuona zimekwama na hata alipotumiwa ujumbe kupitia watu wake wa karibu alikataa.

Ili kuimarisha ulinzi wa mpaka wa Mashariki mwa Serengeti, Waziri Kigwangalla amewaondoa Askari wote wa kituo cha Geti la Kleins kwa kuwa wamekuwa wakitumika na mwekezaji huyo ambaye ana uhusiano wa Karibu na Prof. Songorwa na alikuwa na uhusiano ya karibu na Prof. Maghembe, Lazaro Nyalandu, balozi Kagasheki na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa zamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527