CHADEMA YAMTAKIA KILA LA HERI KATAMBI....YAWASIHI CCM KUMTUMIA KADRI WATAKAVYOONA ANAFAA


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema chama hakina mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi ambaye ametangaza kujiunga na CCM kwa kuwa ni haki ya Kikatiba.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi leo Jumanne baada ya Katambi kuhamia CCM, Dk Mashinji, “sisi kama chama msimamo wetu tuliuweka tangu madiwani walivyoanza kuondoka, tukaweka msimamo wazi kwamba, suala la mtu kuondoka kwenye chama au kubaki ni suala la Katiba ya nchi ambayo inampa mtu uhuru wa kuhama na kwenda kwenye chama anachotakana.”

Amesema kuwa haoni sababu ya kumzuia mtu kuondoka kwa kuwa mtu anapoamua kwenda sehemu yoyote anakuwa na matarajio.

Pia, Dk Mashinji amesema anamtakia heri (Katambi) na kuwataka CCM kumtumia katika sehemu ambavyo wanaona anafaa kutumika kwa faida ya Watanzania wote.

“Hatuna mgogoro wowote na kimsingi mimi nimtakie tu heri (Katambi) na wakipenda (CCM) wamtumie kwenye eneo watakaloona anafaa kutumika kwa faida ya Watanzania wote,” amesema

Hata Hivyo, Dk Mashinji amesema kuwa walikuwa wanamuandaa Katambi asaidie chama hicho kwenye kitengo cha sheria.

“Alikuwa anamalizia masomo yake ili awe wakili na tulikuwa tumeshaanza kumuandaa ili atusaidie kwenye kitengo cha sheria ndani ya chama,”

Katambi ametangaza leo kujiunga na CCM mbele ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) unaofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Na Emmanuel Mtengwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527