BABA WA WATOTO 14 AJIANDAA KUFANYA MTIHANI WA KUMALIZA DARASA LA SABA


NB-Picha haihusiani na habari hapa chini

AMA kweli elimu haina mwisho. Hilo limethibitishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ambaye pia ni baba wa watoto 14 mkazi wa wilaya ya Kamuli, John Bosco Mutebe anayejiandaa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi Novemba, mwaka huu.

Mutebe (44), ataungana na wanafunzi wenzake 128 wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kyeera, Kata ya Namwendwa kufanya mitihani. 

Jumatano iliyopita, baba huyo wa mabinti 11 na watoto watatu wa kiume ambaye ni kiongozi Kanda ya Bwaguusa, alishiriki ibada maalumu ya kuombea wanafunzi wa darasa la saba iliyofanyika Kanisa Katoliki Namwendwa na kuongozwa na Padri Fredrick Wobeera.

Mutebe ambaye pia ni Katekista katika mji mdogo Ngandho wilayani Buyende, alienda shuleni Februari mwaka huu akiomba aruhusiwe kufanya mtihani wa darasa la saba baada ya kukatisha masomo darasa la sita mwaka 1989. 

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sam Caleb Opio anasema: “Kwa kuwa ni kiongozi wa eneo hili, tulijua ana ziara ya kawaida. Lakini alishangaza kusema anataka kurudia darasa la saba.”

Mutebe alisema kutokana na kukosa sifa za kielimu, amekosa nafasi nyingi kanisani na ajira katika mashirika yasiyo ya Serikali huku akikiri anajiona amefanya makosa akiwa madarakani, sababu kubwa ikiwa kukosa elimu ya kutosha.

“Ninaheshimika na nina uelewa mkubwa wa mambo, ndiyo maana ninashikilia ofisi ya umma, lakini siku zote nimekuwa nikijisikia vibaya kutokana na elimu duni,” alisema Mutebe anayeamini atafaulu na kuingia kidato cha kwanza mwakani akiapa kusoma kwa bidii na hatimaye awe mtaalamu wa kilimo kwa kuwa tayari ni mkulima na anapenda kilimo.

Akiwa mwenye furaha, anasema anashukuru kutimiza ndoto ya kuhitimu darasa la saba, jambo ambalo kwa wengi lilionekana sawa na ndoto hasa kwa kuwa tayari ana familia kubwa. Mwalimu wa darasa analosoma Mutebe, Francis Balimisa Kapere, amesifu juhudi na nidhamu yake akisema licha ya umri na hadhi yake kama kiongozi wa Serikali, ni mtaratibu, msikivu, ana uwezo mkubwa darasani na hakosi vipindi.

Wanafunzi wanzake wamemwelezea kuwa ni mtu anayejituma katika masomo na kwamba anawazidi wengi kwa uwezo wa darasani. Mama mzazi wa Mutebe, Rosemary Nantume, anasema kama si ulevi wa baba yake kiasi cha kumfanya akose ada za watoto, mwanaye huyo angefika mbali kielimu, lakini kutokana na mazingira ya familia, alikatisha masomo yake.

IMEANDIKWA NA KAMULI - HABARILEO UGANDA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527