AUAWA KWA KUCHOMWA KISU NA MKE WAKE AKIWA KWA MCHEPUKO

Mkazi wa Mtaa wa Kamando katika Kata ya Igunga Mjini wilayani Igunga mkoani Tabora, Masumbuko Stephano (39) amefariki dunia papo hapo baada ya kuchomwa kisu na mkewe Christina Elias (30) kwa wivu wa mapenzi.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kamando, Julius Kitundu alisema mauaji hayo yamefanyika Novemba 6, mwaka huu saa 7:15 usiku katika Mtaa wa Kamando. 

Kitundu alidai Stephano alichomwa kisu wakati akiwa kwa hawara yake, Happiness William (28) mkazi wa Mtaa wa Kamando.

Alidai mke wa marehemu alimfuata mume wake baada ya kugundua yuko kwa hawara yake, ambako alifika na kugonga mlango kisha kuingia ndani na kumchoma kisu mumewe upande wa kushoto katika eneo la moyo kisha mumewe kuanguka na kupoteza maisha.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Habilo Mhagama alikiri kupokea mwili wa marehemu Stephano, saa nane usiku wa Novemba 6 mwaka huu. 

Dk Mhagama alisema uchunguzi wa awali unaonesha mtu huyo alipoteza maisha kutokana na damu nyingi kuvuja kutokana na kisu alichochomwa kwenye moyo.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Igunga wakisubiri ndugu kuuchukua. 

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kuuawa kwa Stephano, na kuongeza kuwa baada ya polisi kupata taarifa, walifika eneo la tukio na kumkamata mke wa marehemu akiwa na kisu chake.

Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi na kuongeza kuwa upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Imeandikwa na Lucas Raphael - Habarileo Igunga 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527