RAIS MAGUFULI ATAJA MSHAHARA WAKE...ASEMA HAKWENDA IKULU KUUZA SURA

Rais  Dk. John Magufuli amesema tangu alipoingia madarakani hajapandisha mishahara ya watumishi wa umma na  hatapandisha kwa sababu  anawatumikia Watanzania kwanza.

Kauli hiyo aliitoa   Dar es Salaam jana alipofungua Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ambao uliwakutanisha mameya na wenyeviti wa halmashauri nchini.

Rais Magufuli alieleza umuhimu wa ALAT katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mikakati yake kwa Watanzania.

Aliahidi kushughulikia changamoto za uhaba wa watumishi katika halmashauri na ucheleweshwaji wa ruzuku ya miradi ya maendeleo.

Aweka wazi mshahara wake
Katika mkutano huo, Rais Magufuli pia alitaja mshahara wake anaolipwa kuwa ni Sh milioni tisa kwa mwezi.

“Watu walikuwa wanafanya ‘board meeting’ Dubai na wakienda kule wanapandisha mshahara mpaka Sh milioni 40, mimi mshahara wangu ni Sh milioni tisa. Naeleza ukweli. Watu walikuwa wanafanya kufuru,” alisema.

Akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, Mei Mosi mwaka huu, Rais Magufuli aliahidi nyongeza ya kawaida ya mishahara na kuwapandishia madaraja wafanyakazi wanaostahili.

“Watumishi 9,932 walikuwa na vyeti feki, watumishi hewa walikuwa 19706, hivyo kama Serikali ingeongeza mishahara ina maana watumishi hawa pia wangefaidika na fedha ambazo hawakustahili kuzipata,”  alisema Rais Magufuli.

Pia alisema wafanyakazi 12,000 ‘waliotumbuliwa’ kwa vyeti feki hawawezi kumpenda na ndiyo maana wanapiga kelele kupitia mitandao ya  jamii kwa sababu  naye hahitaji kupendwa nao.

“Watu 12,000 waliotumbuliwa kwa vyeti feki hawawezi kunipenda na hao ndiyo wanaopiga kelele kwenye mitandao huko. Tanzania ina watu milioni 52 sasa hawa (12,000) hata hawanisumbui, nikiwaona ‘I just enjoy them’ hata sishtushwi na wanaolalamika.

“Ukimtumbua mtu jipu hawezi kufurahi akipona ndiyo ataanza kuelewa,”alisema.

Pensheni za watumishi hewa
Rais Magufuli aliagiza Sh bilioni 38 zilitokana na waliokuwa watumishi hewa zirudishwe serikalini.

“Zile pensheni zote za watumishi hewa zirudishwe serikalini, Sh bilioni 38 zirudishwe serikalini. Likizo hewa, likizo za uzazi hewa. Tunachukua hatua lakini ni kwa Taifa la Watanzania. Tulikuwa tunaenda kubaya, kuzimu,” alisema.

Benki Ufisadi
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema kulikuwa na benki moja   nchini ambayo ilipata hasara ya asilimia sita na hata ilipoongezewa fedha ilipata hasara zaidi.

“Ikapata hasara zaidi ikaongezewa hela sasa ikapata hasara ya asilimia 11 ikaongezewa hela ikapata hasara zaidi asilimia 22. Sasa tumeifunga.

“Watu kama hawa hawawezi kutupenda na mimi sitaki wanipende ilimradi napendwa na watanzania. Sikuja kuuza sura, nimependwa na mke wangu inatosha,”alisema.

Alisema kuna  benki makao makuu yake yalionekana Dar es Salaam lakini imefunguliwa Marekani na   hata wataalamu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hawakuligundua hilo.

“Kuna benki makao makuu yake yako Dar es Salaam lakini ikafunguliwa kule Marekani. Wataalamu wa BoT hawakugundua haya na fedha ambayo ipo kwenye hiyo benki haizidi asilimia tano,” alisema Rais Magufuli.

Pembejeo hewa
Alisema kwenye halmashauri 140, kulikutwa na pembejeo hewa za kilimo zenye thamani ya Sh bilioni 57.9.

“Hata Chato kwetu kulikuwa na huu uozo pembejeo hewa za thamani ya Sh bilioni 1.5.

“Wanafunzi hewa 65,000 kutoka elimu ya msingi mpaka chuoni. Wanafunzi hewa wanaopokea mikopo walikuwa 8500.

“Ungekuwa mimi umekuta li-Tanzania liko hivi, uozo kila kona ungefanyaje? Ningekuwa Mhehe ningejinyonga, ningesema “Swela,”  alisema.

Alisema wakati anaingia madarakani alikuta mikoa mingi inasumbuliwa na kipindupindu lakini baadaye yalipelekwa madawa.

Pia alisema   bei ya mbolea ya kupandia imeweza kushuka, mathalani katika Mkoa wa Lindi kutoka Sh 100,00 hadi  Sh 51,000.

Alisema wapo watu ambao wanalalamika fedha imepotea na kwamba wanaolalamika ni wale ambao walizoea vya bure.

“Apartment zilikuwa zimepangishwa mtu ana washikaji 10 na wote anawatunza, wengine hadi baa walikuwa wanalipia viti kwamba kila siku lazima akae hapo. Watumishi wengine walikuwa wanasafiri kila wiki, wanabadilishana mabegi pale airport,”alisema Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments