MAPYA YAIBUKA KUHUSU BABU WA MIAKA 60 ALIYEFARIKI AKIJAZWA NGUVU ZA KIUME KWA PAMPU YA BAISKELI



MZEE Joseph Sahani (60) ambaye amefariki duniani akiwa kwa mganga wa kienyeji akifanyiwa dawa ya kuongeza nguvu za kiume, imebainika kwamba alikuwa na wake wawili, watoto zaidi ya 10 na ameacha utajiri wa ng’ombe zaidi ya 50.

Mwili wa Mzee Sahani aliyefariki dunia Jumapili jioni umezikwa katika Kijiji cha Ipango jirani na Kijiji cha Nzoza mahali alipozaliwa katika Kata ya Salawe Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga. Alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga wa kienyeji, Robert Mkoma ambaye anaishi wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nzoza, Shija Kulwa na Mariamu Kuhenge walimueleza mwandishi wa habari hizi kuwa mganga huyo siyo mkazi wa kijiji hicho, bali hutembelea maeneo mbalimbali kwa madhumuni ya kutafuta wateja na kuwapatia huduma ya matibabu.

Kulwa alisema Sahani alipewa taarifa na rafiki yake, Pastori Sitta ambaye alimkaribisha mganga huyo ili afanye matibabu kwa wenye matatizo ya kuishiwa nguvu za kiume na siyo mara yake ya kwanza kufika katika kijiji hicho.

“Mganga huyu siyo mara yake ya kwanza kufika katika kijiji hiki kwani alikwisha kuja na kumtibu mwanaume mmoja aliyeishiwa nguvu za kiume na kuanza kujisifia mitaani kuwa amepona, ndio Mzee Sita alipomfuata Mzee Sahani baada ya kuwa alimueleza naye ana tatizo la kukosa nguvu za kiume na kumhakikishia mganga huyo anaweza kumtibu vizuri tatizo lake,” alidai mkazi huyo wa Nzoza.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nzoza, Masalu Msalaba alisema alipewa taarifa na baadhi ya wananchi kuhusu kifo cha Mzee Sahani, kwamba alikuwa akipatiwa matibabu kwa mganga wa kienyeji ndipo alipochukua hatua ya kuwapigia askari Polisi wa Kituo cha Salawe.

Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu alisema mganga huyo alifika kwa mara ya kwanza kwenye familia ya Mzee Sitta na kumtibu mwanawe aliyekuwa akidaiwa ana tatizo la kukosa nguvu za kiume na alimtibu huku watu wakiamini alimponyesha baada ya yeye na mkewe kukaa miaka mingi bila kupata mtoto na hatimaye akapata mtoto.

“Mganga huyo ameonekana kuaminika na baadhi ya wananchi wa vijiji vya kata hii baada ya kusikia amerudi tena katika familia hiyo akitokea kwenye mji wake Kwimba mkoani Mwanza kwa lengo la kudai deni lake la uponyaji baadhi ya watu walielezana kuwa mganga yupo na huyo mzee kujitokeza kwa kushawishika kuwa atapona matokeo yake kupoteza maisha,” alieleza diwani Buyugu. Mzee Sahani alifariki kwa mganga wa kienyeji Mkoma wakati akipatiwa matibabu ya kupata nguvu za kiume kwa kuwekewa dawa aina ya unga sehemu za siri iliyoingizwa kwa kutumia pampu ya baiskeli.

IMEANDIKWA NA KARENY MASASY, SHINYANGA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments