Baada
ya Askofu wa Kanisa Katoliki nchini kusikika akidai Katiba mpya ndio
kipaumbele cha sasa kwa wananchi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Dar es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo amewataka waumini wa
Kanisa hilo na Watanzania kwa kuyachukulia maoni hayo kuwa si msimamo wa
Kanisa Katoliki.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki hii, Kadinali Pengo amesema kuwa kauli iliyotolewa
hivi karibuni na Askofu wa Jimbo la Rulenge, Ngara mkoani Kagera,
Severine Niwemugizi ni maoni binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki
nchini.
Mwadhama
Kadinali Pengo amesisitiza hilo wakati akitoa ufafanuzi juu ya
sintofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa Kanisa
hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.
“Napenda
kutamka moja kwa moja kwamba huo sio msimamo wa kanisa na hauwezi kuwa
msimao wa kanisa kwa sababu sisi tunataratibu zetu za kuishauri Serikali
au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.
Pengo
amefafanua kuwa kutokana na nafasi ya Uaskofu aliyonayo Askofu
Niwemugizi, kauli yake inaweza kutafsiriwa kuwa ndio msimamo wa Kanisa
Katoliki au wa Jimbo la Rulenge, Ngara lakini kimsingi kauli ile imekosa
vigezo vya kuichukulia kama msimamo wa Kanisa au Jimbo anakotoka.
Akizungumzia
juu ya suala la katiba mpya ambalo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa
wanajaribu kuligeuza kuwa ajenda kuu kwa sasa, Kadinali Pengo alisema
yeye binafsi kipaumbele chake ni kuona huduma za jamii kama zile elimu
na afya zinaendelea kuboreshwa kwa kasi kama ambavyo Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Dkt. Magufuli ilivyoanza kufanya.
“Mtu
akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni katiba mpya inabidi
anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa
au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya katiba mpya. Kwangu mimi katiba ni
kitu ambacho kije baadae, si cha haraka, Pengo"
“Wanasiasa
wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya katiba. Wasiache
watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu
ya katiba,” Kadinali Pengo amesisitiza.

Social Plugin