ALIYEPIGWA CHINI KWENYE UCHAGUZI CCM, ADAI WAGOMBEA WOTE WALITOA RUSHWA

Mgombea uenyekiti wa CCM wilayani ya Babati, mkoani Manyara Gabriel Bukhay ameeleza hadharani jinsi wagombea walivyotumia rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi.

Abdillah Sogora alishinda uchaguzi huo.

Akizungumza baada ya kutangazwa matokeo kwenye uchaguzi huo uliofanyika Jumanne, Bukhay alisema yeye na wagombea wenzake wote walitoa rushwa kwa kuwa wapigakura walikuwa wanawaomba rushwa kwa kutumia simu.

“Kama ni rushwa, tumetoa wote hakuna mtu atakayekuwa nje kwenye tukio hili la kutoa rushwa. Siyo mimi au siyo mzee,” alisema Bukhay.

“Hata mimi nikionyesha meseji kwenye simu yangu, utakuta ‘mzee tunakupenda lakini kwenye mkutano tunakujaje’ hayo yamepita tujenge chama chetu.”

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo wa marudio, mbunge wa viti maalum, Martha Umbullah alisema kura halali kwa wajumbe wote ni 777, hakuna kura iliyoharibika na Bukhay alipata kura 378 wakati Sogora alishinda kwa kupata kura 399.

Awali, uchaguzi huo ulilfanyika Ijumaa iliyopita kwa kuwa na wagombea watatu akiwemo Michael Taxara ambaye alijilitoa na hivyo kushindwa kupata mshindi baada ya wagombea hao wawili kutopata zaidi ya nusu ya kura.

Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Edna Hyera alisema hakuna mgombea aliyekamatwa na rushwa na chama hicho kinafuata taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi huku wakipinga na kukemea utoaji wa rushwa kutokana na mfumo mpya wa uchaguzi.

Hyera alisema chama hicho kimebadili mfumo wa uchaguzi kwa kuwa hata mgombea akiomba nafasi majina huwa kwenye bahasha.

Akizungumza baada ya ushindi, Sogora aliwashukuru wanachama hao kwa kumchagua tena kuwa kiongozi wao na akawaahidi kuwa ataendelea kuwatumikia kwa moyo mmoja kama awali, ila waendelee kumpa ushirikiano wa kutosha kama mwanzo.

“Mnatambua uwajibikaji wangu kwenu na uadilifu. Naichukia rushwa na mtu ambaye sishiriki kwa namna yoyote ile vitendo vya rushwa, hivyo nitaendela kupiga vita vitendo hivyo kwa lengo la kuimarisha chama chetu,” alisema Sogora.

“Wanachama wote wa CCM wa Wilaya ya Babati vijijini nawapenda na vikwazo vyote tulivyovipitia kwenye uchaguzi huu, tusameheane kwa kuwa tulipeana maneno mabaya na makali huku wengine wakisema huyu hayupo kwenye kambi yako na yule akisema huyu hayupo na wewe.”

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Mogasa Mogasa alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo za rushwa zilizotokea kwenye uchaguzi huo.

“Siwezi kuzungumza zaidi kuhusu suala hilo ila ni kweli tupo kwenye uchunguzi zaidi wa tuhuma hizo,” alisema.

“Siwezi kulifafanua zaidi kwenye vyombo vya habari kwa kuwa ni mapema mno kuzungumza kiundani. Sina zaidi la kuongeza.”

Chanzo: Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments