MBOWE: HOFU YA TUNDU LISSU KUPOTEZA MAISHA INAPUNGUA


Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe amefunguka na kusema kuwa ile hofu iliyokuwepo Mbunge Tundu Lissu aliyeshambuliwa na risasi kuwa huenda angepoteza maisha imezidi kupungua na kudai madaktari wanatoa matumaini makubwa hali yake inaimarika.


Freeman Mbowe amesema hayo leo kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii na kusema kuwa Mbunge huyo sasa anaweza kuzungumza japo anaendelea kupatiwa matibabu na kudai pia ataendelea kufanyiwa upasuaji mwingine, aidha Mbowe amewataka wananchi kutosikiliza taarifa za watu wengine kuhusu hali ya mgonjwa na kusema taarifa rasmi juu ya hali ya mgonjwa itatolewa na wao ambao wapo na mgonjwa Nairobi Kenya. 

"Kuhusu hali ya Mhe. Lissu, kwa sasa ile hofu ya kupoteza maisha imezidi kupungua, madaktari sasa wanatoa matumaini makubwa kuwa hali yake sasa inaimarika. Yale yote yaliyokuwa yanatishia pengine uhai wake, usalama wake, yamepungua kwa kiasi kikubwa na madaktari wanatoa matumaini makubwa. sasa hivi, Mhe Lissu anaweza kuzungumza, nimezungumza nae, japo bado anapatiwa matibabu na ataendelea kwenda 'theatre' kwa ajili ya upasuaji na kutibu majeraha mbalimbali aliyoyapata. Anazungumza na anatoa salamu kwa Wanaafrika Mashariki, anatoa salamu kwa Watanzania, niseme tu kwamba sisi ambao tuko nae muda wote ndo tunajua hali halisi ya mgonjwa" alisema Freeman Mbowe
Mbali na hilo Freeman Mbowe amedai kuwa Mbunge huyo hana athari zozote zile kwenye kifua chake kama ambavyo baadhi ya taarifa zinasema kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kudai Mwanasheria Mkuu huyo wa CHADEMA yupo imara. 
"Mhe. Lissu hana 'infection' ya kifua, kwa sasa yuko vizuri yuko imara, bado ni 'critical' lakini bado yuko stable. Tuendelee kumuombea kila siku, wakati wote, aweze kupona kwa haraka na kuruhusiwa kutoka hospitali" alisema Mbowe
Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa kwenda jijini Nairobi Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata, ambapo mpaka sasa yuko huko kwa matibabu. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527