MBOWE AMETOA KAULI HII KUHUSU MAENDELEO YA TUNDU LISSU

Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe amefunguka mapya kuhusu hali ya Mbunge Tundu Lissu ambaye sasa anapatiwa matibabu nchini Kenya, Mbowe amedai wao wanatoa taarifa ya maendeleo ya Tundu Lissu kulingana na madaktari wanavyowaambia.

Freeman Mbowe amesema kuwa wao hawawezi kusema chochote nje ya wataalam hao ambao ndio wenye ujuzi wa kumtibu na kujua hali ya mgonjwa kwa kuwa ndiyo watu ambao wanakaa naye muda mrefu na kutambua maendeleo yake.

"Sisi tunatoa taarifa za maendeleo ya Lissu kulingana na Madaktari wanavyotuambia, hatuwezi kusema chochote nje ya wataalam hao, kwa kuwa ndio wenye ujuzi wa kumtibu na kujua maendeleo ya mgonjwa husika, Unajua ahueni humtokea mgonjwa taratibu taratibu na ndivyo inavyotokea kwa Lissu, ingawa sisi wote tuna hamu apone mara moja aje aendelee kupigania haki za wanyonge kama alivyokuwa akifanya" alisema Mbowe

Aidha kiongozi huyo amezidi kuwaomba Watanzania kuzidi kumuombea Tundu Lissu na kuendelea kuchangia gharama za matibabu kwa kiongozi huyo kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno na wao kama chama peke yao hawawezi hivyo wameomba Watanzania kuendelea kuchangia ili kiongozi huyo aendelee kupata matibabu na aweze kupana na kurejea nchini akiwa salama.

"Kupona kwa Mhe. Lissu ni mpango wa Mungu, nawaomba Watanzania wenzetu waendelee kumuombea kwa Mungu pamoja na kuchangia gharama za matibabu, kwa kuwa gharama zake ni kubwa ambazo chama pekee hakiwezi kuzimudu bila ya misaada kutoka kwa watu mbalimbali" alisisitiza Freeman Mbowe

Mbunge Tundu Lissu yupo mjini Nairobi Kenya kwenye matibabu kufuatia kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa na kwenda Kenya kwa matibabu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527