MABASI YAPIGWA TOCHI USIKU KWA MWENDOKASI MOROGORO


Mabasi saba ya abiria yamekamatwa na kutozwa faini kwa kosa la mwendokasi na kutofuata sheria za usalama barabarani huku wakihatarisha maisha ya abiria.

Kamatakamata hiyo ambayo imesimamiwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Fotunatus Muslim akiwa na timu ya viongozi na askari mkoa wa Morogoro imefanyika usiku wa kuamkia leo.

Zoezi la ukamataji mabasi hayo limefanyika eneo la Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, zoezi lilichukua takribani masaa mawili ambapo mabasi hayo yamezuiwa kuondoka mpaka asubuhi huku yakitozwa faini.

Kamanda Muslim amesema jeshi hilo halitakubali kuona maisha ya watanzania yakipotea kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.

Amesema kikosi hicho cha usalama barabarani kimeahidi kupambana na madereva wa mabasi ya abiria hasa nyakati za usiku kwani ndio wamekuwa wakiendesha kwa mwendokasi huku wakidai serikali muda huo inakuwa imelala.

Mabasi ya abiria zaidi ya saba yanayofanya safari kati ya mkoa wa Mara (Musoma) Dar es salaam, na Mwanza- Dar es salaam yamekaguliwa na kutozwa faini.

Muslim amesema madereva wengi wamekuwa wakifuata sheria za barabarani nyakati za mchana kwa kuhofia kukamatwa kutokana na tochi zilizopo na inapofika nyakati za usiku madereva hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuendesha kwa mwendo kasi.

Akizungumzia dhamira ya Polisi Muslim amesema ni kuwalinda raia na mali zao na kuwataka askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema doria ni endelevu na sasa itakuwa kwa nchi nzima kwa usiku na mchana huku akiwataka madereva hao kuacha kudanganyika kwa madai kuwa tochi usiku hazifanyi kazi usiku na kwamba tochi sasa zitakamata mpaka usiku.

"Nimekuja na slogani ya Kamata hii ni kwa wale madereva wasiotii na kufuata sheria na tutapambana nao kila wakati na nyakati zote na hiyo itasaidia abiria kusafiri salama na matumizi ya barabarani kuwa bora," amesema kamanda Muslim.

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Leon Mwete aliyekuwa katika moja ya basi yaliyokamatwa eneo hilo la Dumila amesema zoezi hilo ni zuri na linafaa kuendelea.

Amesema hii itapunguza ajali za barabarani na kwamba kwa sasa uendeshaji wa madereva wengi ni mzuri ukilinganisha na zamani.

Naye kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro Boniface Mbao ameeleza kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu ataendelea kusimamia na kufanya oparesheni za usiku na mchana kama maelekezo yaliyotolewa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527