JINSI MADIWANI WALIOFUNGA BARABARA GEITA WALIVYOTAWANYWA NA JESHI LA POLISI GEITA


Baadhi ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wakiwa kwenye Barabara ambayo inatoka mgodi wa dhahabu wa Geita GGM wakati wa shughuli za kuwatawanya viongozi hao pamoja na wananchi ambao walikuwa wameandamana.
Wananchi na madiwani wakiwa wameweka Mawe kabla ya kutawanywa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita,Elisha Lupuga akiwa kwenye kikao wakati alipokuwa akielezea namna walivyofukuzwa na jeshi hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mwl,Herman Kapufi akizungumza na kutoa maelekezo ya namna ya kufanya wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya 
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akiwasisitiza kutulia na kuachana na ghasia wasubiri meza ya mazungumzo na Naibu waziri wa Nishati na madini siku ya Jumatatu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo akisisitiza kutokukubaliana na madiwani juu ya tukio ambalo wamefanya siku ya leo. Picha kwa hisani ya Maduka Online.

*****
Jeshi la Polisi Mkoani Geita limelazimika kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi za moto hewani kwa ajili ya kuwaondoa waandamanaji waliokuwa wakiongozwa na madiwani wa halmashauri mbili ambazo ni ya mji na Wilaya ya Geita.

Madiwani hao walikuwa wametanda kwenye barabara ya mgodi huo wakizuia magari kuingia na kutoka Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita (GGM),wakishinikiza kulipwa deni wanaloidai GGM kiasi cha zaidi ya Dola Bilioni 12.65

Tukio hilo limetokea leo (jana) majira ya saa mbili na nusu asubuhi wakati madiwani hao na wananchi wakiwa wamefunga barabara ya mgodi wakishinikiza kulipwa deni hilo kufuatia maazimio ya kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichokeiti juzi.

Azma ya kukata mawasiliano ya barabara na vyanzo vya maji zilianza saa 10.00 usiku ambapo madiwani waliweka mawe katika njia kuu za kuingia mgodini humo na kwenye chanzo cha maji kilichopo Nungwe.

Baadhi ya madiwani wamesema kuwa walikubaliana juzi kwenye vikao vya chama ngazi ya wilaya na mkoa pamoja na baraza maalum kuwa watafanya maandamano ya amani kwa lengo la kushinikiza kudai deni hilo huku wakilaani kitendo cha jeshi hilo kutumia nguvu kubwa.

"Tulikubaliana kwenye vikao ngazi ya chama wilaya ,na mkoa na baraza maalum la madiwani na uongozi wa wilaya pamoja na mkoa unafahamu kuwa leo tunaandamana kudai haki lakini cha kushngaza askari polisi wametutawanya kwa mabomu",alisema Kaparatus.

Kabla ya kutawanywa waaandamanaji hao,Mbunge wa jimbo la Geita Bw. Joseph Kasheku Msukuma alisema amesikitishwa na Kamanda wa Polisi kumtuhumu kuwa yeye ndiye mchochezi mkuu wa mgogoro huo.

“Nashangaa sana RPC anakuwa na chuki na mimi kwani kuwa Mbunge ni tatizo kwani ubunge alinipa yeye hata kama nikiacha ubunge nina maisha yangu na awezi kusema kuwa ccm ni kielele yani kweli sisi ni kielele”,alisema Msukuma.

Ameongezea kuwa kiasi cha fedha zinazodaiwa zinatakiwa kulipwa kwani zimekuwa za muda mrefu na zinaweza kusaidia katika swala la maendeleo.

Hata hivyo amemtaka Kamanda Mponjoli kuomba radhi kwa Chama Cha Mapinduzi ccm na kwa serikali kwa ujumla kutokana na kauli mbaya alizotoa, akiongeza kuwa ameidhalilisha chama hicho.

“Kwa kauli hiyo inadhihirisha wazi kuwa Polisi wanakuwa na upande wakati wanapoenda eneno la kazi na hilo halitakiwi na kwa kutuuliza kwa dhihaka iwapo sisi ni CCM ama siyo, hiyo kauli ni mbaya sana kwani sisi tulikuwa tukidai haki ya kodi hiyo kwa niaba ya wananchi wetu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga, ambaye aliwalaumu madiwani hao kwa kitendo cha kukata bomba la maji katika chanzo cha maji cha Nungwe, aliingilia kati suala hilo akashauri kuwa ni vyema shauri hilo likamalizwa kwa kutumia busara kwa manufaa ya wana Geita.

“Waheshimiwa Madiwani tuweke mbele hekima na busara, tuweke mbele huduma za jamii, za mgodi wa GGM na wananchi kwa jumla ziendelee kwa amani hebu tuwe watulivu wakakti tukitafuta suluhu, kudai haki ni sawa lakini ni njia zipi mnatumia kuzidai, tuache kudai haki kwa njia ya fujo ya aina hii kwani sheria za nchi haziruhusu,”alisema.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Geita Mwl Herman Kapufi amesema suala hilo limefikishwa katika wizara ya nishati na madini na kwamba jumatatu ya wiki ijayo Naibu waziri akiambatana na Kamishina wa madini watafika mkoani Geita kukutana na pande zote kwaajili ya kutafuta suluhu

“Hata hivyo tumewasiliana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Mendrad Kalemani juu ya suala hili ambapo tumekubaliana kukutana jumatatu ijayo, akiambatana na Kamishna wa madini ambapo tutakaa nao pamoja na GGM ili kujadili suala hili”,alisema Kapufi.

Licha ya ahadi hiyo ya Viongozi kutoka kwenye wizara husika, Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande akaomba kutoa taarifa kwa mkuu wa wilaya kuwa kamanda wa jeshi la Polis mkoani humo anawatetea wawekezaji hasa GGM ambao wameshindwa kulipa fedha za kuharakisha maendeleo ya Mkoa

Naye Mkuu wa mkoa huo Meja jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga,amesema njia pakee ya kumaliza mgogoro huo ni kufuata sheria,kanuni na taratibu bila kuathiri shughuli za kijamii na huduma kwa wananchi na kwamba njia iliyotumiwa na madiwani kudai haki yao si sahihi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita,Mponjoli Mwabulambo alisema hayupo tayari kuomba radhi kwani swala hilo na mkusanyiko huo umefanyika kinyume cha sheria na kwamba hakuna lugha ambayo ametumia kukikashifu chama cha mapinduzi CCM.

IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527