MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA ABAKWA HADI KUFA

Mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya msingi Kapanga  iliyopo katika kijiji cha Kapanga kata ya Katuma Tarafa ya Mwese Wilaya ya Tanganyika Veronica Lucas (13)   amekutwa akiwa amekufa baada ya kubakwa hadi kufa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa kwenye shimo la kolongo. Mwandishi wa Malunde1 blog,Walter Mguluchuma anaripoti.



Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Katavi Benedict Mapujila alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa kumi na moja na nusu jioni .


Alisema siku hiyo ya tukio Veronica aliondoka nyumbani kwao kama kawaida yake kwenda kwa ajili ya masomo katika shule ya msingi aliyokuwa akisoma ya Kapanga .

Alieleza kuwa marehemu baada ya kwenda shuleni hakurudi tena nyumbani kwao hali ambayo iliwafanya wazazi wake wapate shaka kwani hakuwa na tabia ya kutorudi nyumbani kwao.

Siku iliyofuata wazazi wake na marehemu walikwenda kufuatilia shuleni na hawakuweza kumkuta hali ambayo ilizidi kuwatia hofu zaidi na waliamua kwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji hicho.

Viongozi wa kijiji pamoja na wananchi wa kijiji hicho waliamua kuanza kumtafuta kwenye maeneo mbalimbali ya kijiji hicho kwa muda wa kutwa nzima pasipo kukata tamaa.

Kaimu Kamanda alisema ilipofika saa kumi na moja na nusu ya jioni waliukuta mwili wa marehemu Veronica ukiwa umetupwa kwenye shimo la kolongo huku akiwa tayari ameshapoteza maisha   baada ya kubakwa na watu wasiojulikana na sehemu zake za siri zikiwa zimeharibika vibaya.

Alisema chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo wa kike kilitokana na kubakwa na kisha kuvuja damu nyingi na kusababisha kifo hicho cha kinyama kikatili.

Alisema  mpaka sasa hakuna mtu wala watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo na jeshi la polisi linaendelea na msako wa kuwasaka watu waliohusika na tukio hilo la kinyama.

Mwili wa marehemu  baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari walikabidhiwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi ambayo yaliyofanyika kijijini hapo siku iliyofuata.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog- Katavi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments