CHADEMA : WATANZANIA WASIWE WATU WA KUTOA PONGEZI KAZI YA MAKINIKIA HAIJAISHA


 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kuwa kipo tayari kumuongoza Rais John Magufuli katika kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo madini, huku kikiwataka wananchi kuishauri serikali kuchukua hatua kwanza badala ya kuipongeza kuhusu sakata la Makinikia.

Akizungumza na akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Katibu Mkuu Chadema, Dkt. Vincent Mashinji amedai kuwa, hatua anazochukua Rais Magufuli kuhusu Makinikia ziko kinyume na Ilani ya CCM ambapo katika ukurasa wake wa 26-28 haikuzungumzia kurekebisha sheria na mikataba ya madini, na kwamba ilani ya Chadema kwenye ukurasa wake wa 57-59 inaonyesha namna ya kuiongoza vizuri sekta ya madini.

“Rais hatafaulu vita hii kama serikali yake itaendelea kutubagua au kutosikiliza sauti ya upande wa pili. Pia watu wasiwe wa kutoa pongezi kabla kazi haijaisha. Kama tunatakiwa kulipwa trilioni mia, wajue kwamba za kwetu ni asilimia 4 tu, na hii ndiyo matokeo ya mikataba tuliyoilaani kila siku. mrabaha wetu ni asilimia 4 huku wawekezaji kwenye pesa hizo za kwao ni  96%,” amesema.

Hata hivyo, Dkt. Mashinji ametaja hatua kadhaa ambazo amedai kuwa kama Rais Magufuli atazichukua, zitamuwezesha kushinda vita aliyoianzisha ikiwemo, kuleta katiba mpya, kurudisha ‘Bunge Live’ ili watanzania wawaone wabunge ambao ni mawakala wa uporaji rasilimali za nchi, ili wawahuku katika chaguzi zijazo.

“Kama anataka kulifanikisha hili kwa uwazi arudishe bunge live, arudishe mikutano ya hadhara sisi tusimame tuwaambie watanzia, tuwataje mafisadi wako wapi ili twende kupambana nao,” amesema.

Hatua nyingine alizotaja, ni kuzitoa hadharani ripoti zote mbili za makinikia, kuweka wazi mikataba ya siri iliyopitishwa na Bunge, kuwachukulia hatua waliohusika na upotevu wa rasilimali, pamoja na kuyafanyia kazi maoni ya wapinzani.
Na Regina Mkonde

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments