MTOTO WA MIAKA MIWILI AUAWA KWA KUNYONGWA NA BABA YAKE WA KAMBO

Picha haihusiani na habari hapa chini


MTOTO Agatha Raphael(2) aliyekuwa akiishi katika kijiji cha Mao wilayani Kalambo mkoani Rukwa amefariki dunia baada ya kunyongwa na baba yake wa kambo.Mwandishi wa Malunde1 blog,Sumbawanga Walter Mguluchuma anasimulia kisa hiki.

Tukio la kunyongwa kwa mtoto huyo lilifanyika Mei 16 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni kijiji cha Mao kata ya Mbuluma tarafa ya Matai,wilaya ya Kalambo, mkoa wa Rukwa.

Akitoa taarifa za tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema kabla ya mtoto huyo kuuawa kwa kunyongwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha akiwa na baba yake wa kambo.

Alisema  mama mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Anisia Kasiti(22) alikwenda mashineni na kumuacha nyumbani mtoto wake huyo.

Kamanda alisema siku kadhaa kabla mtuhumiwa kufanya mauaji hayo alisikika akiongea kuwa lazima amuue yule mtoto kwani siyo wake.

Baada ya kauli hiyo ambayo ilitishia kuuawa kwa mtoto Agatha ndipo alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha na mnamo Mei 17,2017 ambapo mama wa mtoto huyo alikwenda kutoa taarifa katika uongozi wa kijiji na juhudi  za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio.

 Mei 18,2017 mama wa marehemu alikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi Matai kuhusu kupotea kwa mwanae Agatha Raphael na jalada la uchunguzi lilifunguliwa ili kumchunguza baba wa kambo kutokana na kauli aliyoitoa hapo awali.

Baada ya taarifa hiyo polisi walimshikilia mtuhumiwa na huku juhudi za kumtafuta mtoto zikiwa zinaendelea.

Kamanda Kyando alisema Mei 24,2017 majira ya 11:50 jioni mkazi wa kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Aron Mwanambogo, aligundua kuwepo kwa mwili wa marehemu Agatha shambani kwa mtuhumiwa ukiwa umelala chali kwenye kijito kilichopo ndani ya shamba hilo.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu iligundulika kuwa mtoto huyo alikufa kutokana na kukosa hewa baada ya kunyongwa.

Mtuhumiwa bado anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.


Mwili wa marehemu mtoto Agatha umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Kyando alitoa wito kwa wananchi mkoani humo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kama kuna matatizo ya kifamilia na ndoa ni vizuri wanandoa hao wakasuruhishana kupitia kwa viongozi wa ukoo, dini na ikishindikana ni bora kutengana kuliko kufanya mauaji kama ya mtoto Agatha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527