Picha: WANAUME SHINYANGA WAJITOKEZA KWA WINGI KUTAHIRIWA,47,500 WAPATA TOHARA BURE



Huduma za tohara kwa wanaume zimeshamiri mkoani Shinyanga ambapo zaidi ya wanaume 47,500 wamenufaika na huduma hiyo katika kipindi cha Mwezi Oktoba 2016 hadi Machi 2017 kupitia kampeni ya Tohara Kinga ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kujikinga na maambukizi ya VVU. 


Kampeni hiyo inaendeshwa na serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Intrahealth International kwa ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Maambukizi ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Centre for Diseases prevention and Control (CDC). 

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Mratibu wa kudhibiti maambukizi ya VVU mkoa wa Shinyanga Dkt. Mawazo Amri Saleh amesema serikali imekuwa ikishirikiana na shirika la Intrahealth International katika kuendesha huduma ya tohara kwa vijana na wanaume kuanzia miaka 10 na kuendelea. 

Alisema tangu waanze kampeni hiyo katika halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga mwezi Oktoba 2016 mpaka mwezi Machi 2017, zaidi ya wanaume 47,500 wamepatiwa huduma ya tohara bila malipo yoyote. 

Alisema huduma hizo zilitolewa kupitia mfumo wa huduma vituoni na huduma za nje ya vituo zinazotolewa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali zipatazo 50 katika wilaya zote za mkoa wa Shinyanga. 

“Lengo la kampeni hii ni kuwapatia huduma wanaume 95,900 katika kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 lakini mpaka sasa tumefikia asilimia 50 ya lengo lililokusudiwa”,alieleza Dkt. Saleh. 

Alizitaja faida za tohara kwa wanaume kuwa ni pamoja na kujikinga na maambukizi ya VVU kwa asilimia 60,kuwa msafi,kujikinga na magonjwa ya ngono,kujikinga na kansa ya kichwa cha uume na kuwakinga akina mama kansa ya mlango wa kizazi. 

Aliongeza kuwa zoezi la tohara kwa wanaume linazidi kuwa na mwitikio mzuri kwani wanaume wengi wamekuwa wakijitokeza kupata huduma ya tohara. 

“Tunatoa shukrani kwa shirika la IntraHealth kwa ushirikiano mzuri wanaoutoa katika utoaji huduma za tohara mkoani hapa,tunaamini kuwa kutokana na mipango IntraHealth tuliyopanga kwa mkoa na wilaya lengo la mkoa la kufikia asilimia 80 ya tohara kwa wanaume wote mkoani hapa litafanikiwa”,aliongeza Dkt. Saleh. 

Naye Mshauri wa Kiufundi wa masuala ya tohara mkoa wa Shinyanga kutoka shirika la Intrahealth International, Dkt. Innocent Mbughi alisema mbali na mkoa wa Shinyanga hivi sasa shirika hilo linatekeleza pia mradi wa tohara ya mwanaume katika mikoa ya Mwanza, Geita, na Simiyu ambapo katika kipindi cha mwezi Novemba 2016 hadi Machi 2017, zaidi ya wanaume 127,000 wamepatiwa huduma za tohara. 

Dkt. Mbughi alisema wamefikia asilimia 50 kwani lengo ni kuwapatia huduma za tohara wanaume wapatao 256, 529 katika kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 katika mikoa hiyo ambapo pia huduma ya upimaji wa hiari wa VVU inatolewa.

Dkt. Mbughi alibainisha kuwa shirika la Intrahealth International kwa ufadhili wa Mfuko wa rais wa Marekani wa Kupambana na Maambukizi ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Centre for Diseases prevention and Control (CDC) limekuwa likishirikiana na serikali kupitia wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, kitengo cha kuzuia kuenea kwa maambukizi ya VVU (NACP), kamati za afya za mkoa na wilaya na wadau wengine wa afya katika kutoa huduma bora za tohara kwa wanaume. 

Serikali ya Tanzania imeandaa mpango wa kitaifa wa kutekeleza huduma za tohara ili kufikia lengo la kitaifa la asilimia 80 kutoka asilimia 72 kwa sasa (THIMS report 2011) ambapo kipaumbele kimeelekezwa kwenye mikoa yenye viwango vya chini vya huduma za tohara na maambukizi ya VVU.

Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Katavi, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Ruvuma na Mara wilaya ya Rorya.

Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde ametembelea baadhi ya vituo vinavyotoa huduma ya tohara katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu na Kahama Mji ametusogezea picha 22 za matukio
Mratibu wa kudhibiti maambukizi ya VVU mkoa wa Shinyanga Dkt. Mawazo Amri Saleh akielezea namna serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoshirikiana na shirika la Intrahealth International kuendesha kampeni ya tohara bure kwa vijana na wanaume kuanzia miaka 10 na kuendelea. Alisema jamii nyingi nchini Tanzania hufanya tohara ya mwanaume kwa sababu za kijadi na kiimani lakini sasa wanaume wengi wamehamasika kupata huduma hiyo. 
Mshauri wa Kiufundi wa masuala ya tohara mkoa wa Shinyanga kutoka shirika la Intrahealth International, Dkt. Innocent Mbughi akielezea namna wanavyoendesha kampeni ya tohara kwa wanaume katika mfumo wa huduma za nje ya vituo (outreach) katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu na Kahama Mji lililoanza Machi 15,2017 hadi Aprili 11,2017 ambapo mpaka Aprili 6,2017 zaidi ya wanaume 10,000/= wamepatiwa huduma ya tohara bure.
Dkt. Mbughi alisema takwimu za wanaume 47,500 kufanyiwa tohara kuanzia Oktoba 2016 hadi Machi 2017,zinatokana na huduma iliyotolewa kupitia mfumo wa huduma vituoni na huduma za nje ya vituo ambapo jumla ya hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali zipatazo 50 katika wilaya zote za mkoa wa Shinyanga zimefikiwa. 
Aprili 6,2017-Hapa ni katika zahanati ya Mwabomba iliyopo katika kijiji Mwabomba kata ya Idahina halmashauri ya Ushetu wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambapo huduma ya tohara kwa wanaume katika mfumo wa nje ya huduma za kudumu za tohara imeanza Machi 15 hadi Aprili 11,2017-Pichani ni vijana na wanaume wakisubiri kupata huduma ya tohara
Mhudumu wa Tohara katika zahanati ya Mwabomba Lydia Mabagala akizungumzia huduma ya tohara waliyoanza kuitoa tangu Machi 15,2017 mpaka Aprili 11,2017 ambapo mpaka Aprili 6,2017 jumla ya wanaume 880 walikuwa wamepatiwa huduma ya tohara katika zanahati ya Mwabomba. Katika kufanikisha utoaji wa huduma za tohara,jumla ya watoa huduma wa afya wapatao 166 wa kada mbalimbali za afya waliopata mafunzo juu ya namna bora za utoaji wa huduma za tohara kwa wanaume wameshiriki katika kutoa huduma. 
Mtaalam wa afya akimfanyia tohara mwanamme aliyefika katika zahanati ya Mwabomba kupata huduma ya tohara bure.Umuhimu wa tohara ya mwanaume umeongezeka tangu pale Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilipopitisha matokeo ya kisayansi yaliyoonesha kwamba tohara ya mwanaume ina changia kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa wanaume hadi kwa asilimia 60. 
Vijana wakielezea kuhusu namna watakavyofaidika na huduma ya tohara waliyofanyiwa katika zahanati ya Mwabomba .Kulia ni Mhudumu wa tohara katika zahanati ya Mwabomba, Lydia Mabagala 
Bwana James Medard akielezea umuhimu wa mwanamme kufanyiwa tohara 
Bi. Rebeca Daudi akielezea namna alivyohamasika na kuamua kumpeleka mtoto wake katika zahanati ya Mwabomba ili apatiwe huduma ya tohara
Vifaa vinavyotumika kufanyia tohara 
Afisa kutoka Intrahealth International, Andrew Richard akionesha mashine inayotumika kusafishia vifaa vinavyotumika kufanyia huduma ya tohara
Hapa ni katika ofisi ya afisa mtendaji wa kijiji cha Tumaini kata ya Wendele halmashauri ya Mji wa Kahama ambapo zoezi la kuwafanyia tohara wanaume linaendelea. Kulia ni Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akitoa elimu ya tohara kwa vijana na wanaume waliofika katika kituo hicho kupata huduma ya tohara 
Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akionesha mfano wa uume ambao haujafanyiwa tohara wakati akitoa elimuya tohara
Huduma ya tohara ikiendelea katika kituo cha Tumaini kata ya Wendele
Uume kabla ya tohara na baada ya tohara
Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akielezea umuhimu wa mwanamme kufanyiwa tohara. Alisema kwa kipindi cha Machi 15 mpaka Aprili 6,2017 jumla ya wanaume 706 wamefanyiwa tohara katika kituo hicho 
Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akionesha mfano wa uume ambao haujafanyiwa tohara na uume ambao umefanyiwa tohara.Kushoto ni Maria Mwakisyala ambaye ni miongoni mwa watoa huduma ya tohara katika kituo hicho cha Tumaini 
Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akionesha mfano wa uume ambao haujafanyiwa tohara 
Zoezi la kuandikisha vijana na wanaume ili wafanyie tohara likiendelea
Mtoa huduma za tohara Nchama Samson akimpima presha mkazi wa kijiji cha Tumaini aliyefika katika kituo hicho 
Ndaki Lucas akielezea faida za tohara kwa mwanamme 
Helena Gabriel aliyemleta mtoto wake kupata huduma ya tohara akielezea faida ya tohara na kulishukuru shirika la Intrahealth International kuendesha zoezi hilo.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527