KAULI YA ASKOFU NKOLA NA WACHUNGAJI BAADA YA KUFUKUZWA KAZI KANISA LA AICT

Aliyekuwa askofu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Dkt. John Kanoni Nkola akizungumza na Malunde1 blog kanisani baada ya askofu mkuu wa kanisa hilo kutangaza kuwachukulia hatua viongozi watano wa kanisa hilo akiwemo askofu Nkola-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Aliyekuwa katibu mkuu wa  kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Jakobo Mapambano ambaye ni miongoni wa wachungaji waliovuliwa uchungaji akizungumza na waandishi wa habari
Waliokuwa wachungaji wa kanisa la AICT,Jakobo Mapambano(kushoto) na Dkt. Meshack Kulwa( kulia) wakimsikiliza askofu mkuu wa kanisa la AICT Silas Kezakubi akitangaza uamuzi uliochukuliwa na kanisa kuwawajibisha viongozi wa tano wa kanisa hilo

Askofu mkuu wa kanisa la AICT Silas Kezakubi akitangaza uamuzi wa kuwachukulia hatua viongozi watano wa kanisa hilo.
*******

Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) limemstaafisha askofu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Dkt. John Kanoni Nkola na kumtaka kujiuzulu nafasi ya uaskofu askofu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Mwanza John Bunango kwa kushindwa kusimamia vizuri fedha za kanisa kwa ajili ya kuendesha shule ya sekondari Bishop Nkola iliyopo mjini Shinyanga.


Mbali na maaskofu hao kuchukuliwa hatua,pia wachungaji watatu wa kanisa hilo wamevuliwa nafasi ya uchungaji ambao ni Emmanuel Isaya,Dkt. Meshack Kulwa na Jakobo Mapambano aliyekuwa katibu mkuu wa kanisa hilo dayosisi ya Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa waumini wa kanisa   la AICT Kambarage mjini Shinyanga wakati wa ibada ya Jumapili,Askofu mkuu wa kanisa la AICT nchini Tanzania askofu  Silas Kezakubi alisema uamuzi wa kuwachukulia hatua viongozi hao umetokana na kikao cha baraza la utendaji la sinodi kuu AICT.

Askofu Kezakubi alisema viongozi hao wamelitia aibu kanisa kwa kushindwa kusimamia vizuri  fedha kiasi cha shilingi milioni 400 zilizokopwa katika benki ya CRDB mwaka 2008 kwa ajili ya kuendesha shule ya sekondari Bishop Nkola iliyoanzishwa mwaka 2009 na kusababisha shule hiyo kupigwa mnada Februari 23,2017 baada ya kushindwa kurejesha deni.

“Baada ya kuuzwa kwa shule hiyo tuliitisha kikao cha dharura cha baraza la utendaji, tuliunda tume huru kuchunguza jambo hili na baada ya kumaliza uchunguzi wao, walileta taarifa na tumeamua kuchukua maamuzi kwa mujibu wa taarifa hiyo na katiba ya kanisa letu”,alifafanua askofu Kezakubi.

Alisema kupitia uchunguzi huo ilibainika kuwa kuuzwa kwa shule hiyo kunatokana na kwamba kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha za mkopo kutoka benki na fedha za harambee mbili zilizofanyika kanisani hapo na tatizo la kutotoa taarifa kwenye vikao vya ngazi za juu kwani ngazi za juu zilishtukizwa tu kuwa shule imeuzwa.

“Kwa sababu ya mzigo wa uongozi na yeye kama msimamizi, baraza la utendaji liliamua kumuomba askofu Nkola astaafu kuanzia sasa na alipopokea barua hakuwa na maneno ya kukataa na sisi tunampongeza kuchukua moyo huo kwa kuwajibika”,alieleza askofu Kezakubi.

Alisema kosa la askofu Nkola ni kushindwa kusimamia watendaji wake vizuri ili jambo hilo lisitokee vile  vile alikuwa hajatoa taarifa kwenye mabaraza ya juu  kuhusu jambo hilo.

“Askofu Nkola ameumia kwa sababu ya watendaji wake kutokuwa waaminifu kwani kazi nyingi zinawaangukia watendaji,askofu hashughuliki na fedha, ana majukumu yake,lakini sasa mambo yanapotokea na kwa sababu yeye ndiyo msimamizi lazima awajibishwe”,aliongeza askofu Kezakubi.

Aidha alisema baraza hilo limechukua hatua pia kwa watendaji waliokuwa katika ofisi ya askofu Nkola ambapo lilimuomba aliyekuwa katibu mkuu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga John Bunango ambaye sasa ni askofu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Mwanza naye ajiuzulu nafasi yake ya uaskofu.

Alisema askofu Bunango anachukuliwa hatua kwa kutosimamia vizuri fedha za kanisa shilingi milioni 400 za mkopo kutoka benki ya CRDB na za harambee iliyoendeshwa kanisani hapo na waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye.

Askofu huyo aliongeza kuwa Bunango pia alishindwa kusimamia urejeshaji wa mkopo huo kwa sababu hata wakati akiwepo kulikuwa na matatizo na alishindwa kutumia wataalam katika kuvunja baadhi ya mikataba ambayo alikuwa anaisimamia mwenyewe na kusababisha hasara kubwa katika kanisa.

Aidha Bunango aliruhusu ongezeko kwenye mikataba mbalimbali bila kufuata utaratibu wa kuongeza gharama za miradi hiyo.

Katika hatua nyingine baraza lilimvua uchungaji katibu mkuu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Jakobo Mapambano kwa kushindwa kupeleka taarifa sahihi katika vikao vya juu tangu kuanza kwa tatizo la shule.

“Mchungaji Mapambano pia alishindwa kusimamia vizuri mapato ya shule na fedha za harambee nyingine iliyofanyika kanisani na kushindwa kukabidhi nyaraka alizoombwa na tume iliyoundwa na baraza la utendaji kwa ajili ya uchunguzi,na kuweka rehani magari magari mawili ya kanisa bila kuomba kibali cha baraza la udhamini”,aliongeza askofu huyo.

Alisema pia baraza hilo lilimuondoa  katika uchungaji Emmanuel Isaya ambaye alikuwa kwenye kitengo cha elimu ambapo aliidhinisha malipo kinyume na mamlaka yake na kushindwa kusimamia ujenzi wa majengo ya shule ambayo yako hali ya chini na hayajakamilika.

Hali kadhalika baraza hilo lilimwondolea uchungaji Dkt. Meshack Kulwa kwa makosa ya kimaadili na kushindwa kusimamia vizuri ujenzi wa uzio wa shule ambao una ubora wa chini.

Alisema tume inaendelea kufanya kazi na yeyote atakayeguswa lazima achukuliwe hatua za kinidhamu.

“Jambo hili limeleta aibu katika kanisa letu,kama mtu akiharibu hekalu la mungu naye mungu atamharibu mtu huyo kwani hekalu la mungu ni takatifu,kanisa ni hekalu la mungu na yeyote aliyechukua mali ya kanisa arudishe kabla ya kuharibikiwa na mungu,naomba tuendelee kuliombea kanisa”,alieleza askofu Kezakubi.

Akizungumza na Malunde1 blog askofu mstaafu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Dkt. John Kanoni Nkola alisema amewajibishwa kutokana makosa yaliyofanywa na watendaji wake wa chini kwani hata tume iliyoundwa kuchunguza haikuona kama amehusika na ubadhirifu wa fedha katika kanisa.

“Kanisa lina kanuni,sheria na taratibu zake kama kiongozi niliyekuwa naongoza kanisa nimepokea maamuzi yaliyochukuliwa kwa moyo mweupe kabisa,nimeona kulikuwa na madhaifu ya kiuongozi,nilitakiwa kustaafu tarehe 25 Mei 2017,nimestaafu kabla nitaendelea kulitumikia kanisa kwa lolote watakalohitaji niwatumikie kama mstaafu”,alisema askofu Nkola.

Nao wachungaji waliovuliwa nafasi hiyo walisema wanakubaliana na hatua iliyochukuliwa kwa kanisa lina sheria,taratibu na kanuni zake.

Aliyekuwa katibu mkuu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga mchungaji Jakobo Mapambano alikiri kutenda makosa yaliyotajwa na kuongeza kuwa matatizo katika shule hiyo aliyarithi mwaka 2010 kutoka kwa aliyekuwa katibu wa kanisa hilo Bunango ambaye sasa ni askofu wa kanisa hilo dayosisi ya Mwanza aliyeombwa kujiuzulu nafasi hiyo.

Aidha Mapambano alisema matatizo katika kanisa hilo yanachangiwa na kukosekana kwa ushirikiano baina ya viongozi na waumini wa kanisa hilo.

Askofu mkuu wa kanisa la AICT nchini Tanzania askofu  Silas Kezakubi  ndiyo atakuwa msimamizi wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga mpaka pale atakapopatikana askofu mwingine kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Nkola.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527