MBUNGE CHADEMA ANUSURIKA KIPIGO JENGO LA CCM


MBUNGE wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema), amenusurika kipigo kutoka kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupita na gari lake mbele ya jengo la Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Majala alipita eneo hilo, gari lake likiwa limefungwa bendera mbili za Chadema, huku akiwa amefungulia kwa sauti kubwa muziki wa kunadi sera za chama chake.

Tukio hilo lilitokea wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli akiwa ndani ya jengo hilo akiongoza Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala.

Sekeseke hilo lilianza saa 7 mchana kwa Majala na wenzake wawili kupita mara tatu na gari hilo mbele ya jengo hilo wakati mkutano ukiendelea hali ambayo ilionekana kuwakera wana-CCM, hivyo kuamua kulisimamisha.

Gari hilo lenye namba T 152 CDA lilisimamishwa wakati likitokea barabara ya One Way karibu na Benki ya NMB.

Baada ya kusimamishwa, dereva wa gari hilo, Stephen Masawe na kijana mmoja aliyekuwamo ndani ya gari, waliamrishwa washuke kisha wakaanza kuhojiwa sababu za kupita mara kwa mara katika eneo hilo wakiwa wamefungulia muziki kwa sauti kubwa na kupeperusha bendera za Chadema.

Wakati dereva huyo na mwenzake wanatoa ufafanuzi, Majala alikuwa kimya ndani ya gari.

Majadiliano ya vijana hao na wana-CCM hayakuchukua muda mrefu kwani ghafla makada wengine wa CCM walivamia eneo hilo na kuanza kuwashushia kipigo.

Wakati vijana hao wawili wakipata kipigo, bado Majala alikuwa kimya akishuhudia wenzake wanavyoshughulikiwa na kuchaniwa nguo zao.

Hali hiyo iliwalazimu askari walikuwapo katika lango la kuingia uzio wa jengo la CCM Makao Makuu kuingilia kati na kuwazuia makada wa CCM kuwashambulia vijana hao.

Baada ya kutuliza mashambulizi, askari waliwachukua vijana hao pamoja na Majala na kuwapeleka kituo cha polisi kwa mahojiano.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alphonce Mbasa, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa wamepigwa na kuchaniwa mashati yao.

“Ni kweli tukio hilo lipo, waliopigwa zaidi ni dereva Stephen Masawe na mtumishi wa chama kanda, Justin William ambao kwa sasa taratibu zinafanyika ili wapelekwe hospitali, lakini mbunge aliokolewa na polisi,” alisema Mbasa.

Mwenyekiti huyo alieleza sababu za gari hilo kupita katika eneo la mkutano wa CCM kuwa walikuwa wanatoka benki ambako mbunge alikwenda kuchukua pesa ili kuwasaidia watumishi hao kupeleka gari gereji kwa matengenezo.

Mbasa alisema gari hilo lilikuwa limefungwa bendera kubwa mbili ambazo wakati wote hutumika katika magari hayo maarufu kama M4C na ndiyo sababu likatambulika kwa haraka kuwa ni la Chadema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Na RAMADHAN HASSAN-MTANZANIA DODOMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527